Home / Uncategorized / News & Events / Semina katika Seminari Ndogo ya Bikira Maria Malkia wa Mitume – Ushirombo, Kahama.

Semina katika Seminari Ndogo ya Bikira Maria Malkia wa Mitume – Ushirombo, Kahama.

Ni ukweli usiopingika ya kuwa zizi lisilokuwa na ndama liko hatarini kuisha. Ukweli huu hujidhihirisha pia katika wito wa upadre, yaani, kama Kanisa mahalia na la kiulimwengu halina vijana wanaoitikia wito wa kuwa mapadre basi utume wa Kanisa uko hatarini kwa siku za usoni. Tunamshukuru Mungu kwamba kwa Kanisa Mahalia la Tanzania ziko jitihada nyingi sana zinafanyika ili kuhamasisha miito ya upadre na utawa. Moja katika jitihada hizo ni uanzishwaji wa Seminari Ndogo na Kuu. Mfano mzuri wa jitihada hizi ni Jimbo Katoliki la Kahama ambalo linayo Seminari Ndogo ya Bikira Maria Malkia wa Mitume iliyoko Ushirombo.

Katika kushiriki kazi ya malezi ya waseminaristi, ambao ni moja ya wajibu unaoiangukia Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), siku ya tarehe 07 Julai, 2020 ofisi ilipanga safari ya kutembelea Seminari tajwa hapo juu. Katika siku hii ilitolewa Semina maalumu kwa ajili ya waseminaristi na walezi wao juu ya mada mbili, yaani: (1) MAKUZI KATIKA ROHO YA KIMISIONARI na (2) MASHIRIKA YA KIPAPA NA NAFASI YAKE KATIKA KANISA. Semina hii iliandaliwa na kutolewa na Pd. Alfred Stanslaus Kwene ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tume ya Uinjilishaji Taifa.

Tunamshukuru Mungu kwamba Semina hii ilipokelewa vizuri sana na waseminaristi pamoja na walezi wao (mapadre, watawa na waalimu walei). Kwa namna ya pekee waseminaristi walionesha umakini na uhai katika kufuatilia semina hii na hali kadhalika walikuwa jasiri hata kuuliza maswali kwa ajili ya kujifunza zaidi. Tathimini ya haraka haraka inaonesha kuwa, kwa washiriki wengi wa semina hiyo, Shirika pekee la Kipapa walilolifahamu ni Utoto Mtakatifu. Hivyo, ilikuwa fursa nzuri ya kuyatambulisha pia mashirika mengine matatu na kazi zake katika Kanisa. Hali kadhalika, ilikuwa ni nafasi nzuri sana ya kuwaalika waseminaristi na walezi wao kushiriki katika kazi za Uinjlishaji za Baba Mtakatifu kupitia mashirika haya kwa njia ya sala na majitoleo yao. Walikumbushwa ya kuwa mashirika haya hutambulikana kuwa ni mtandao (network) wa kiulimwengu wa sala na majitoleo kwa ajili ya kuungana na Baba Mtakafitu kufanya kazi ya uinjilishaji.

Kwa kuzingatia kuwa baadhi ya waanzilishi wa mashirika haya walikuwa na umri mdogo tu (Mfano, Pauline-Marie Jaricot), hiyo ilikuwa ni fursa ya kuwakumbusha hasa waseminaristi ya kuwa hata katika udogo wao wanao uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika Kanisa. Kwa kufanya rejea katika busara ya Mt. Yosefu Alamano aliyesema: “Uwe Mtakatifu, Mtakatifu Mkubwa sasa” (Be a saint, a great saint, now), mwezeshaji aliwakumbusha waseminaristi wasidhanie kuwa wakati wao bado, bali wanaalikwa waanze sasa kuweka bidii ya kuwa wamisionari na hatimaye watakatifu. Hali kadhalika kwa kuhusianisha maneno hayo ya Mt. Josefu Alamano na umisionari, mwezeshahi aliwaasa waseminaristi wadogo kwa kusema: “Uwe mmisionari, mmisionari mkubwa, sasa” (Be a missionary, great missionary, now). Mwasho alihitimisha kwa kuwatakia neema na baraka katika malezi yao.

Imeandaliwa na Pd. Alfred S. Kwene (Mkurugenzi Msaidizi PMS Taifa)