Home / Uncategorized / News & Events / SEMINA KWA MAKATEKISTA WA CHUO CHA BUKUMBI – JIMBO KUU LA MWANZA

SEMINA KWA MAKATEKISTA WA CHUO CHA BUKUMBI – JIMBO KUU LA MWANZA

Katika kutekeleza sehemu ya majukumu yake, siku ya tarehe 10 Julai, 2020, Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (PMS-TEC) ilifanya ziara katika Chuo cha Makatekista cha Bukumbi kinachomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo Kuu la Mwanza. Lengo mahususi la ziara hiyo ilikuwa ni kutoa semina kwa makatekista. Semina hiyo iliendeshwa na Padre Alfred Stanslaus Kwene ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa PMS Taifa na ilihusu mada kuu mbili, yaani:

(1) MAKATEKISTA NA UMISIONARI KATIKA KANISA na

(2) MASHIRIKA YA KIPAPA NA NAFASI YAKE KATIKA KANISA.

Katika semina hiyo, kwa upande mmoja mwezeshaji alihimiza juu ya makatekista kukua katika roho ya kimisionari kwani Kanisa Katoliki ambalo wanategemea kufanya kazi ndani yake ni la kimisionari kwa hulka yake. Pamoja na kuwa kila mmbatizwa anaitwa kuwa mmisionari, lakini ni zaidi sana kwa Katekista. Kwa upande mwingine, alitoa mafundisho ya msingi juu ya Mashirika ya Kipapa, yaani, Shirika la Kipapa la Kimisionari la Uenezaji Imani, Shirika la Kipapa la Kimisionari la Mt. Petro Mtume, Shirika la Kipapa la Kimisionari la Utoto Mtakatifu na Shirika la Kipapa la Kimisionari la Umoja wa Kimisionari. Alikazia juu ya chimbuko la kila shirika, kukua na kuenea kwake na hali kadhalika nafasi yake leo hii. Aidha, alikazia kuwa uzoefu unaonesha kuwa kwa sehemu nyingi ni Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu ndilo linafahamika zaidi na hata kudhaniwa kuwa ndio shirika pekee. Hivyo, aliwasihi makatekista kuyafahamu vema na kushiriki katika kufundisha ukweli halisi juu ya mashirika haya.

Itakumbukwa kuwa chuo cha Bukumbi ni cha pekee sana kwa Tanzania, kwani tofauti na vyuo vingine, kimeandaliwa kupokea wanafunzi wa ukatekista kifamilia, yaani hupokea mke, mume na watoto — walio chini ya miaka saba na kina uwezo wa kupokea familia zisizopungua 26. Makatekista wawapo chuoni huishi pia kifamilia na hufanya huduma nyingine vivyo hivyo (mfano kazi za mikono za uzalishaji, kazi za ndani, kula, n.k.). Pia, kwa watoto ambao tayari wamekwishaanza shule na wanaambatana na wazazi wao kuja chuoni basi huombewa nafasi katika shule ya msingi iliyo jirani ili kuweza kuendelea na masomo yao. Tena, kwa akinamama wanaolazimika kuwasindikiza waume zao chuoni hapo hupata pia fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali za ujasiliamali (kama vile ushonaji, kilimo, ufugaji, n.k.). Kwa muundo huu, pande zote mbili za wanafamilia huondoka zikiwa zimenufaika sana kwa mmoja kupata elimu ya ukatekista na mwingine kujifunza juu ya ujasiliamali.

Ni matumaini ya Tume ya Uinjilishaji Taifa ya kuwa semina iliyotolewa kwa makatekista hao itazaa matunda yanayotarajiwa. Kwa kuzingatia kuwa ilihudhuriwa na wanafunzi na wenzi wao, hawa kwa hakika wanategemewa wawe mstari wa mbele katika kuhamasisha kwa waamini wengine moyo wa umisionari na nafasi ya Mashirika ya Kipapa katika Kanisa.

Imeandaliwa na Padre Alfred S. Kwene (Mkurugenzi Msaidizi PMS Taifa)