Home / Uncategorized / News & Events / Ziara ya Maaskofu katika Seminari Kuu ya Ntungamo – Bukoba

Ziara ya Maaskofu katika Seminari Kuu ya Ntungamo – Bukoba

Seminari ya Mt. Anthony wa Padua Ntungamo imepokea ugeni wa  Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa jimbo kuu la  Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania,  alieambatana na Askofu Anthony Lwagen wa jimbo katoliki la Mbulu. Wamefika mahali hapa kwa ajili ya ziara ya kichungaji,  ikiwa ni utaratibu waliojiwekea wa kutembelea taasisi zilizopo chini ya Baraza hilo la Maaskofu. Maaskofu wamepokelewa vizuri na Askofu wa jimbo la Bukoba alieambatana na uongozi wa seminari chini ya Baba Gombera Frumence Ghumpi.

Katika ziara hiyo ya siku mbili kuanzia 15/05/2021 hadi 16/05/2021, maaskofu wamepata fursa ya kusali ibada ya Misa Takatifu ya Jumapili ya 7 ya Pasaka, ambapo Askofu Lwagen aliongoza ibada ya Misa Takatifu huku Askofu Mkuu Nyaisonga akitoa homilia. Katika homilia yake Askofu Mkuu Nyaisonga, amesisitiza kuzingatia umoja, upendo, na ushirikiano baina ya wanajumuiya wote wa seminari Kuu ya Ntungamo. Akitumia msemo unaosema, kazi ni kipimo cha utu, amewaasa kufanya kazi kwa bidii na kujituma hasa katika kuitumia vizuri miradi iliyopo seminarini katika kustawisha seminari.

Katika Malezi ya Seminari Askofu Mkuu Nyaisonga, ameeleza jinsi malezi fungamano yalivyo ya msingi ndani ya seminari, akisisitiza kuwa katika nyanja kuu za malezi yaani (Kitaaluma, Kiroho, kichungaji, na kiutu), zote kwa pamoja zinapaswa kuzingatiwa katika uwiano sawa. Akiongelea changamoto mbalimbali, Baba Askofu Mkuu, amesisitiza kuwa uwezo wa akili zetu ni mkubwa sana ajabu, ambao kadri mtu anavyopambana na changamoto mbalimbali ndivyo anavyotumia akili yake na kwa namna hiyo akili kuendelea kukua.

Katika ziara hiyo, maaskofu wamepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Waseminaristi na walezi kwa nyakati tofauti. Wametembelea maeneo mbali mbali ya seminari ikiwemo miradi ya samaki, Nguruwe, Shamba la Migomba, nk. pia waliweza kutembelea jengo jipya (bweni) ambalo limejengwa kwa michango iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Imeandaliwa na Frt. Emmanuel Mangu (Seminari ya Ntungamo)