Sala: Kwa Jina la Baba na la Mwana nala Roho Mtakatifu Amina.

Salamu Maria umejaa neema, bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa/ Maria mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu Amina.

Bikira Maria Malkia wa Familia, Utuombee

Kwa jina la baba na la mwana na la Roho mtakatifu amina.

Kutoka hapa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unayenisikiliza muda huu ni mimi Sr Anagladness Mrumah, ambaye ni Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa.

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu kutoka Bunena, leo napenda Kuwaasa Wazazi kuwasaidia Watoto wao kuziishi Amri za Mungu na za Kanisa kwani inaonekana hii ni changamoto kwa wazazi wengi. watoto wanaishia kuzifundishwa hizi amri kwenye mafundisho yao huko kanisani tu, wakifika nyumbani wazazi hawana habari kwamba ndio wanaopaswa kuhakikisha kuwa watoto wanaziishi hizi amri.

 

Wapendwa wasikilizaji, pengine imekuwa sasa ni tabia ya sisi wazazi kuona kuwa ni wajibu wa viongozi wa kanisa kufundisha juu ya amri za mungu na za kanisa kwa watoto wetu, ingawaje hata sisi wazazi tayari tunazifahamu. Haidhuru hata kama ni wajibu wao viongozi wa kanisa kuzielezea kwa watoto wetu, lakini watoto wamekuwa wengi wao wanakengeuka yaani hawazishiki wala kuziishi vyema kwani sisi wazazi tumeshindwa kuwasisitiza ili waweze kuziishi ndani ya familia zetu.

 

Wapendwa wasikilizaji, wengi wetu tunashindwa kuwakazania watoto wetu waziishi vyema amri za Mungu na za Kanisa, kwakuwa sisi nasi tumeshindwa kuziishi. Hii ndiyo sababu tunashindwa kusisitiza, kitu ambacho wenyewe hatukiishi. Kwamfano, amri ya kwanza ya kanisa inayosema, Hudhuria Misa Takatifu na Dominika zilizoamriwa! Sasa kama mzazi mwenyewe mlango wa kanisa anauona kama kituo cha polisi, je, ataweza kumsisitiza mwanae juu ya amri hii ya kuhudhuria misa takatifu? Je kama katika umri huo alionao mzazi hajaona thamani ya maadhimisho ya misa takatifu ambayo ni kilele ya ibada zote, ataonaje ulazima wa kumlea mtoto katika kutambua kwa matendo thamani ya kuhudhuria misa takatifu? Jibu ni haiwezekani kwakuwa mtu hutoa kile alichonacho moyoni mwake. Ndugu zangu kuhusu kuhudhuria misa ama kutokuhudhuria misa kwa mtoto, hilo ni jukumu la mzazi. Kwahiyo tuwahimize waende kanisani, tusisubiri mapadre wakahimize watoto kufika kanisani wakati sisi ndio viongozi wa familia ambao tuna wajibu wote wa kutekeleza jukumu hili. Na ndugu zangu wazazi, niseme tu kwamba, kama sisi tunaonekana kupuuzia mambo haya matakatifu, ndio maana hata watoto mara nyigine wanalegea katika Imani kwani daima mtoto anaangalia na kuiga kile kinachofanywa na mzazi.

 

Vile vile wapendwa wasikilizaji, ni vyema sisi kuwasisitizia watoto wetu hasa wale ambao wameshapata komunyo ya kwanza, kupokea ekaristi ambayo ni amri ya kanisa, tena wakiwa wamejiandaa vyema kwani ekaristi takatifu ni Yesu Kristo mwenyewe. (Rejea Mt 26:26-28) Ni chakula cha kipekee kuliko vyakula vyote tunavyokula katika maisha yetu. Ekaristi takatifu ni uzima wetu, ni dawa ya kiroho. Ingekuwa vizuri kama mzazi angeona njaa ya kiroho kama hakupata nafasi ya kupokea ekaristi takatifu. lingekuwa ni jambo la maana kama mzazi naye angeendelea kumkazia mtoto juu ya thamani ya Ekaristi Takatifu. lingekuwa ni jambo la busara kama mzazi kabla mtoto hajaenda kanisani, angepata wakati wa kumkumbushia namna ya kupokea ekaristi takatifu viganjani. Tena Lingekuwa jambo jema kama mzazi angeweza mara kwa mara kumkumbushia mwanae kumwambia yesu maombi yake wakati anapokula mwili wa Kristo yaani ekaristi katatifu. Sishangai kwamba wengi wetu tunashindwa kuyafanya haya yote kwakuwa sisi nasi hatuioni thamani ya ekaristi takatifu na pengine hatushiriki hii ekaristi.

 

Kwanini, kwasababu eti mzazi ametenda dhambi na hataki kuiungama wazi na hii kumpelekea kukosa huduma hii muhimu ya kiroho. Wengine tumekuwa tukikubali kuchanganywa na madhehebu ambayo yanapinga uwepo wa Yesu ndani ya Hostia Takatifu. Sasa kwakuwa mzazi anakubali kuchanganywa, basi naye anakosa ujasiri wa kuhamasisha wanae juu ya ukuu wa ekaristi takatifu, na hivyo kufanya watoto kukosa mwamko katika kuyashiriki matakatifu. Na pengine mzazi mwingine ni mvivu wa kwenda kanisani na kwahiyo hapati hii nafasi ya kushiriki ekaristi takatifu. Na wengine wanajishikilia sana na shughuli za ulimwengu huu pasipokuona kuwa ipo haja ya kutenga siku moja hii muhimu kwa ajili ya Mungu na hivyo kuweza kuiishi amri ya tatu ya Mungu inayosema, Shika Kitakatifu Siku ya Mungu. (Kumb 5:12)

 

Mbaya zaidi wapendwa wasikilizaji, wengine kwakuwa siku za katikati ya wiki alikuwa amebanwa na shughuli, basi anaona kuwa jumapili niya mapumziko. Ndio ni ya mapumziko ila kwa mkristo mkatoliki mapumziko kwa siku ya jumpili yanaanza mara baada ya kushiriki misa takatifu. Kumbe ndugu zangu wazazi, baada ya mtoto wako kupokea mafundisho juu ya namna ya kupokea ekaristi, shule ya nyumbani ndiyo inapaswa kuchukua mkondo wake wa kuendelea kuhamasisha matakatifu kwa watoto wetu. Vitu hivi tungevifanya sisi wazazi kama majukumu ya mzazi kwa mtoto wake, hakika kiroho watoto wetu wangekuwa mbali. Sasa sisi tumezoea kwamba mtoto akishamaliza mafundisho ya sakramenti husika inatosha, Jambo ambalo si sahihi. Kwa hulka ya mwanadamu ili akili yake iweze kukaa sawa, ni lazima akumbushwe mara nyingi juu ya jambo muhimu, ili jambo lile liweze kumkaa kama sehemu ya maisha yake.

 

Wapendwa wasikilizaji, hebu ona umuhimu wa wewe kumfundisha mtoto wako juu ya kutoa zaka. Pengine utasema kwamba zaka ni fungu la kumi la pato la mtu na mtoto hana pato kwakuwa anakutegemea wewe mzazi. Lakini ndugu zangu wazazi, hebu jaribu kumshirikisha mtoto kwamba kama unampatia shilingi elfu moja, basi mia moja amtolee mungu kama zaka yake. Lengo msingi hapa ni kumzoeza mtoto kufahamu au kupata uelewa huu akingali mdogo ili akishakuwa mkubwa na kumiliki hela yake mwenyewe, awe tayari anajua kuwa kama mwanakanisa anapaswa kutoa zaka kwani hii ni amri ya tano ya kanisa. Tusiwaache hawa watoto wakaziimba tu hizi amri pasipo kuzielewa kwa undani.

 

Kwamfano mtoto kila asubuhi na jioni anaimba amri ya tatu ya Mungu, Ungama dhambi zako walau mara moja kwa mwaka. Lakini tangu mtoto wako alipoungama akiwa anapata komunio ya kwanza, hakuwahi tena kuliona sanduku la maungamo. Kwanini, kwasababu wewe mzazi unaona hilo sio jukumu lako la kujua kwamba mtoto anaendeleaje kiroho. Kumbe katika udogo wake, hata akimpiga mwenzake, akiiba sukari, akitukana watu, ungeweza kumsihi aende kuungama! Hii ingemfanya aiishi amri ya 3 ya kanisa! Familia ni shule jamani, na waalimu ni wewe baba na mama

 

Wapendwa wasikilizaji, kama sisi wazazi tungekuwa tunawasisitiza sana watoto wetu kujihami juu ya uvunjifu wa amri za Mungu kwa mfano amri ya  ya tano ya mungu inayosema USIUE, hakika tusingeshuhudia mauaji ya kiroho ama ya kimwili ambayo yamekuwa yakitendeka hapa na pale, kwani mtu anayethubutu kuua mwingine kiroho kwa maneno yake machafu ambayo yanaweza kumchafua mwingine nahata kushusha hadhi yake, au kimwili yaani kuutoa uhai wake, huyu ni yule ambaye hajui athari ya kuua wala thamani ya utu wa mtu mwingine. Na mtu yeyote anayefanya kitendo hicho ni yule ambaye hakufundwa na wazazi wake na ndio maana anaweza kuona tu kwamba ni jambo la kawaida. Ndio maana wazazi, leo nimeamua nizungumzie juu ya jambo hili kwani tumekuwa tukikariri amri za mungu na za kanisa lakini wengi wetu hatuziweki katika matendo. Ni jukumu letu wazazi kuwasisitiza watoto wetu juu ya kuyaacha yale matendo ambayo mungu ameyakataa kwani hayo ni chukizo kwake. Kama watoto watakuwa wanakuwa na hofu ya Mungu na kuona kuwa jambo baya hawapaswi kulitenda pindi wakiwa wadogo, basi vitendo viovu havitaweze kutendeka katika jamii zetu. Lakini kama tutasubiri makatekista, masista na mapadre wafundishe na halafu itoshe, basi tutakuwa tunapoteza vizazi vya mbele yetu, kwani wahimizaji wa mambo haya ni sisi wazazi ambao tunaweza kufuatilia mienendo yao siku zote kwani wao ni sehemu ya familia zetu.

 

Kipindi hewani ni kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unayenisikiliza muda huu ni mimi, Sr Anagladness Mrumah. Ndugu zangu wasikilizaji leo nimeamua kuwasisitiza wazazi kuhakikisha kuwa wanawahimiza watoto kuzishika na kuziishi amri za Mungu na za kanisa barabara kwakuwa amri hizi baada ya kufundishwa kwenye mafundisho, hazishikwi barabara kwa kuwa wazazi walio wengi hawawahamashishi watoto kuziishi wala kuziishi.

 

Ndugu zangu wazazi, kama sisi wazazi tungewasisitiza watoto wetu juu ya kushikilia amri za mungu tungeweza kuzuia maovu mengi. Kwamfano, kama unaona mtoto ana hali ya udokozi, ingekuwa ni vizuri kumkumbusha kwa kumsisitiza kuwa asirudie tena kwani ni amri ya saba ya mungu. Kwa msisitizo kama anajua kusoma unafungua biblia kabisa aone kwamba ni kweli kumbukumbu la torati sura ya 5:19 Mungu anasema usiibe. Yaani asione tu kwamba ni amri yako wewe unayompa ya kutofanya kitendo kile, bali kwamba ni amri kutoka kwa mungu kwamba kuiba hakuruhusiwi kabisa. Sasa sisi tunalea pasipo kuonyesha rejea kwenye mambo matakatifu ambapo mtoto angeweza kushikilia vizuri zaidi baada ya kujua kuwa mzazi na mungu hawataki jambo la kuiba kwani ni baya. Ndugu zangu hakuna mtu anayeweza kuiba kama katika maisha ya utoto wake aliaswa kwamba jambo hili ni chukizo kwa Mungu. Kwahivyo tuwahimize watoto kuziishi amri za mungu, wasikariri tu.

 

Wapendwa wasikilizaji matendo ya uovu kama yale ya kusema uongo, usaliti kwenye ndoa ama uvunjifu wa ndoa visingekuwapo kama sisi wazazi tungekuwa tuko mstari wa mbele kuwalea watoto wetu katika kushikilia mambo kama hayo. Tazama leo watu wanazushiana uongo hata wa kuingizana jela, au kuua dhamiri za wengine kwa maneno yao ya uongo. Kwanini? Kwakuwa hawana hofu ya Mungu. Wazazi wao hawawazi wala kukaa na kuwahimiza watoto wao kuwa wasijethubutu kuyatenda hata kabla hayajatukia. Wazazi wengine kwa uongo wameshawarithisha watoto wao hadi mtoto anaona uongo ni sehemu ya maslahi au mafanikio yake. Mtoto mwingine anashindwa kutulia kwenye ndoa yake, awe wa kiume ama wa kike kwakuwa mzazi hakuwahi kukemea kabla. Na pengine wazazi nao wanashindwa kuzungumzia hayo kwakuwa baba na mama wote ni wasaliti wa amri hiyo ya mungu. Kwahiyo kwa mantiki hii watoto wanashindwa kushika amri ya nane ya mungu inayosema Usiseme Uongo kwani wazazi hawako tayari kulizungumzia jambo hilo kwakuwa nao wapo kwenye shimo hilo hilo la uongo, wala kukemea juu ya usaliti kwani wamekuwa wakiuendesha usaliti ama bado wameukumbatia.

 

Kwahiyo ndugu zangu wasikilizaji wa Redio Maria na mshirika wake Redio Mbiu, tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa na watoto wetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa amri za mungu na za kanisa zinashikwa. Tukumbuke kuwa mtoto anaposikia na kutenda, jambo hilo linakaa akilini zaidi na hivyo kulichukua kama sehemu ya maisha yake ya kila siku. Kwamfano, kama mtoto amesikia juu ya amri sita za kanisa na halafu mzazi akawa wa kwanza kumsaidia kuziishi kwa kumshirikisha kiutekelezaji, hakika mtoto hata akiwa mtu mzima hataacha kushika amri za kanisa. Ee, ataenda kanisani, atapokea ekaristi kama ameshapokea sakramenti ya ekaristi, atatoa zaka kama mzazi amekuwa akimtolea na kumwelewesha maana yake, na amri zote za kanisa

 

Hali kadhalika, kama mzazi atamsisitiza mtoto wake kushika amri za Mungu, mtoto ataweza kutambua kuwa ni yapi Mungu anamtaka ayafuate na ni yapi anamkataza asiyafanye. Hebu wazazi tusome tena amri za Mungu ambazo zinapatikana katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:1-21 ili tuone maagizo haya kutoka kwa Mungu. Kwa kweli mimi naamini kwamba kama mtoto hazishiki amri za Mungu kwasababu ya uzembe wa mzazi, basi mzazi huyo ndiye anayeathirika kwanza kabla ya jamii. Maana, Amri hizi tumepewa na Mungu tuzishike illi zitusaidie kuishi kwanza kitakatifu na pili kiadilifu katika familia na jamii zetu. Kama hatuzizingatii tutakuwa tunafuga katika jamii watu wezi, waongo, wasio na heshima, wasaliti, washirikina, wauaji na wasiojua wajibu wao ndani ya kanisa lao. Kwa leo ni haya nilipenda wasikilizaji wa Redio Maria na Mshirika wake Redio Mbiu tujikumbushie.

 

Ni mimi mtangazaji wako Sr Anagladness Mrumah kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)