Kwa jina la baba na la mwana na la roho mtakatifu Amina

Atukuzwe baba na mwana na roho mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote na milele amina

Bikira Maria Malkia wa familia, utuombee

Kwa jina la baba…………………..

Wapendwa wasikilizaji, hewani ni mimi Sr. Anagladness Mrumah wa shirika la Masista wa Usambara (COLU). Mimi ni katibu mtendaji wa Utoto Mtakatifu taifa, katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Karibu uu ngane name tangu mwanzo hadi mwisho wa kipindi hiki.

Mada ya leo ni kuhusu sifa za wazazi wawajibikaji

Ndugu zangu wasikilizaji, ni dhahiri katika jamii zetu malezi yamekuwa kila mara yanatofautiana kutoka mtoto mmoja na mwingine, kwasababu ya wahusika wakuu yaani wazazi ambao wapo katika aina tofauti tofauti. Kwa ajili ya hali hii, kwenye jamii kumekuwa na watoto wanaofaidi malezi thabiti kwa wazazi wao, wengine wakiwa wanapokea malezi vuguvugu, huku wengine kukosa malezi kabisa kutoka kwa wazazi wao, ambao wameonekana kuwa na mitazamo tofauti kwenye malezi.

Ndio maana mara nyingi wewe na mimi pengine tunajiuliza, ni kwanini mtoto huyu ana tabia hii, mwingine ile.  Kumbe ni kwasababu ya namna wazazi wanavyojiweka mbele ya watoto wao. Kwamfano, ukikuta mzazi ni muwajibikaji, basi watoto watapata malezi stahiki, mzazi akiwa ni yule wa kuruhusu kila kitu kiende katika familia, basi utakuta watoto nao wanateketea, ukikutana na wazazi wanaowakandamiza watoto kwenye familia, basi ujue hapa utakutana na watoto walioathirika kisaikolojia. Na kwenye familia nyingine kama utakutana na wazazi wazembe na watepetevu basi ujue malezi ya watoto wao yanakuwa na hali mbaya. Wazazi wengine kama watakuwa wapuuziaji wa mambo ujue kila kitu kitaenda kombo kwa watoto. Na kama wazazi wengine ni wale wasinziaji, ndio basi tena, kwenye jamii utakutana na watoto wasio na mwelekeo. Ndugu zangu hizi zote ni aina za wazazi ambao wanaishi katika jamii zetu yaani:

  • Wazazi wawajibikaji
  • Wazazi wa ruksa
  • Wazazi wakandamizaji
  • Wazazi wazembe na watepetevu
  • Wazazi wapuuziaji
  • Wazazi bubu
  • Wazazi wasinziaji
  • Wazazi wenye hatia

Wapendwa wasikilizaji, shabaha yangu ni kuelezea hizi aina za wazazi na sifa zao ili kusudi kila mzazi aweze kujifahamu kuwa je, yeye yupo katika aina ipi. Kama akijitambua kuwa yupo kwenye aina isiyotakiwa katika jamii kwenye kutoa malezi basi na ajinasue huko ili kuwa katika sehemu sahihi. Leo nitaanza kuelezea juu ya aina ya wazazi wawajibikaji kwa kujikita katika kuelezea sifa zao.

Wapendwa wasikilizaji, Wazazi wawajibikaji ni wazazi ambao wanatambua vema wajibu wao na hivyo wako tayari daima kuutimiza wajibu huo wakijua fika kuwa ni katika kutoa malezi bora, wanalijenga Kanisa la nyumbani na taifa la kesho. Wazazi wawajibikaji ni waalimu wa shule hii ya mwanzo kabisa (yaani shule ya malezi). Kipindi kilichopita nimeeleza kuwa familia ni shule ya kwanza kabisa katika kumuunda mtoto kimwili na kiroho. Katika shule hii ya awali kabisa kwa mtoto, nilieleza kuwa, waalimu wa shule hii yaani familia, ni baba mama. Kumbe, kama baba na mama ni waalimu kwenye familia zao, basi kwa hakika hawa ndio wanapaswa  kuangalia nidhamu za watoto wao, afya za watoto wao, makuzi ya watoto wao, taaluma za watoto, Imani thabiti ya kimungu wanayopaswa kuwa nayo watoto wao, kwa kutaja machache.

Ndugu zangu, baba na mama wana wajibu mwingi sana katika familia. Suala la kumlisha na kumvisha mtoto tu halimfanyi mzazi kuitwa kuwa ni muwajibikaji. Uwajibikaji upo kwenye mambo kadhaa katika familia. Pengine ningesema kuwa, familia ni kanisa la nyumbani, na viongozi wa kanisa hili la nyumbani ni baba na mama ambao ndio kwa hakika wanapaswa kuhakikisha uimara na uthabiti wa kanisa hili la nyumbani. Kama Kristo anavyotafsiriwa katika maandiko matakatifu kuwa ni kichwa cha kanisa (Rej. wakolosai 1:18), basi itoshe kusema kuwa wazazi nao wakiwa ndani ya familia ni vichwa katika kuwaongoza watoto wao kumfahamu na kumuishi Kristo.

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji, ni wale wanaotambua kuwa, familia ni shule ya sala, na kwahiyo, muda wote wanahakikisha kuwa watoto wanasali asubuhi, mchana na jioni. Ni wazazi wanaotenga muda wa kusali na watoto wao, ni wazazi wanaofundisha watoto wao kusali, ni wazazi wanaowafundisha watoto wao namna ya kukaa kwa utulivu wakati wa kusali, tena ni wazazi wanaowafundisha watoto wao kusali sala zinazotoka moyoni na si kusali kwa kutimiza wajibu wa kusali, kwani wanaelewa kuwa sala ni maongezi kati ya mtu na muumba wake. Tena, wazazi wawajibikaji ni wazazi wanaohakikisha kuwa wanasali pamoja kama familia wakiamini kuwa wanaposali pamoja Mungu anajiunga nao na kukaa mahali pale kwa wakati ule kama alivyosema; walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao. (Matayo 18:20)

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji ni wazazi wanaotambua kuwa, familia ni shule ya upendo, na kama familia ni shule ya upendo, wanajitahidi kuonyeshana upendo na kuzuia tofauti zao. Wazazi hawa wawajibikaji ambao wanatambua kuwa familia ni shule ya upendo, wanajua kuwa wao ndio waalimu wa somo la upendo kwa watoto wao. Tena upendo kwa Mungu na kwa jirani. Wazazi wawajibikaji wanahakikisha kuwa Watoto wao wanapendana wao kwa wao  katika familia, watoto wanalelewa namna ya kuwapenda majirani, ndugu na watu wote kwakuwa wanaaminishwa kuwa kila mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Rej. kitabu cha Mwanzo 1:27). Wazazi wanaowajibika kuwafundisha watoto wao, watoto wao ni wale ambao wamekuwa daima wenye kujitoa katika majukumu mbalimbali bila ya hata kujibakiza, na ndio maana wamekuwa na sifa makazini mwao. wazazi wawajibikaji katika kutoa shule ya upendo kwenye familia zao, watoto wao wanakuwa wasio na choyo, wakarimu, watoto wao hawana lugha za matusi, watoto wao wanakuwa na mahusiano mazuri na jamii zinaowazunguka, wanakuwa watatuzi wa shida za watu wengine kwa shauri zao zenye tija.

Kadhalika ni watoto wasio na hila katika maisha yao. Daima wazazi wawajibikaji katika kuwafundisha watoto wao juu ya upendo, watoto wao maisha yao yanasambaza harufu ya upendo kwa vizazi vyao. Ndo maana utasikia, ukitaka mke bora, ama mfanyakazi bora ama msimamizi mzuri wa kitu ama jambo fulani, nenda wa watoto wa mzee Joseph. Hii ni kwa sababu ya uwajibikaji mahiri wa wazazi unatengeneza mafanikio ya watoto kwa sasa na baadaye.

Kipindi hewani kipindi ni kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unayenisikiliza ni Sr Anagladness Mrumah wa Shirika la Masista Wa Usambara (COLU). Leo nimependa kuzungumzia juu ya aina ya wazazi kwenye kutoa malezi ambapo aina hizo za kiutoaji malezi zina athari hasi na chanya. Nimesema kuna aina za wazazi kama vile:

  • Wazazi wawajibikaji
  • Wazazi wa ruksa
  • Wazazi wakandamizaji
  • Wazazi wazembe na watepetevu
  • Wazazi wapuuziaji
  • Wazazi bubu
  • Wazazi wasinziaji
  • Wazazi wenye hatia

Lakini katika aina hizi, leo nimeanza na ile aina ya wazazi wawajibikaji ambayo kwa uhalisia ndiyo aina bora ambayo inapaswa kuigwa na kila mzazi katika kutoa malezi.

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji ni wale wanaotoa mafunzo ya utii kwa watoto wao wakijua kuwa, familia ni shule ya utii. Wazazi wawajibikaji ni wazazi wanaoanza kuwafundisha watoto wao utii tangu wakiwa wachanga kwa kutumia ishara na baadaye wanapoendelea kukua wanatumia maneno na matendo yanaomdai mtoto kuwa mtii. Ni wazazi wanaowajibika kuwafundisha watoto wao wawatii wao wazazi kwakuwa hata Yesu anawataka watoto kuwatii wazazi wao; Enyi watoto watiini wazazi wenu (waefeso 6:1-4). Wazazi wawajibikaji wanawafundisha watoto waonyeshe utii kati yao watoto. wazazi wawajibikaji wanawafundisha watoto kutii wakubwa na wadogo. Wazazi wawajibikaji, wanafundishwa watoto wao kuwatii waalimu mashuleni na, Zaidi sana, wazazi wawajibikaji wanawafundisha watoto wao kutofautisha utii mzuri na mbaya wakiwa wanaamini kuwa kuna watu wanaoweza kutumia dhana ya utii na kuwaathiri. Mzazi muwajibikaji anafinyanga kizazi chenye utii.

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji wanafundisha watoto wao somo la uaminifu.  Daima wazazi hawa huhakikisha watoto wao ni waaminifu, wasio na hila, wenye kuridhika na walichokuwa nacho, wanawafundisha watoto wao kuzuia tabia ya udokozi, wanawafundisha watoto wao kuwa waaminifu katika misimamo yao na si kusababisha shida kwa wengine kwa ajili ya kukosa uaminifu. Wazazi wawajiikaji huhakikisha kuwa wanafuatilia taratibu kila hatua ya mtoto ili kuona kama huenda mtoto ana tabia mbaya anayoificha, ili akibaini amrudishe kwenye mstari.

Wapendwa wasikilizaji, Wazazi wawajibikaji ni shule ya fadhila nyingi.  Wanatimiza vema kazi yao wakijua kuwa wanatimiza kwa matendo sehemu ya viapo vyao vya ndoa; (Rej. Mithali 19:18, Waefeso 6:4) yaani kuwalea watoto wao kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake, huku wakiwarithisha watoto wao mila za wazee zilizo njema.

Wapendwa wasikilizaji, Wazazi wawajibikaji daima huwa na muda kwa ajili ya watoto wao. Hufuatilia kwa karibu kama watoto wametimiza wajibu zao katika elimu, au kama wamefanya vizuri katika kazi za nyumbani. Mzazi mwajibikaji humuunda mtu mzimamzima. Haishii tu kuzaa, bali huendelea kumzaa mtoto wake, kimaadili, kiimani, kielimu, kimahusiano na ki-uwajibikaji pia. Wazazi wawajibikaji, huunda watoto wenye kutimiza wajibu pia.

Kwa kuhitimisha Wapendwa wasikilizaji, hii ndiyo aina ya wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto wao. Kwa hakika, nilizozitaja ndizo baadhi tu ya sifa wanazokuwa nazo wazazi wawajibikaji. Ningetamani na wewe msikilizaji wangu kutafakari kwa kina juu ya sifa hizi ili uweze kuwa mwalimu na balozi mzuri wa kusambaza sifa hizi katika jamii inayokuzunguka, kwa njia ya ushauri kwa wazazi wenzako, ili hatimaye watoto ambao ndio kizazi cha sasa na baadaye, waweze kupokea misingi imara itakayowasaidia kuwa watu wenye utu, watu timamu na watu wenye elimu ya malezi kwa watoto wao vizazi baada ya vizazi.

Tumalize kwa sala

Kwa jina la baba na la mwana na Roho Mtakatifu amina

Atukuzwe baba na mwana na Roho Mtakatifu kama mwanzo na sasa na siku zote……

Kwa jina la baba na la mwana na Roho Mtakatifu amina