Kwajina la Baba na la Mwana naa Roho Mtakatifu …

Bwana Yesu tunakushukuru kwa baraka zako unazotujalia siku hata siku. Tunaomba uendelee kuichochea mioyo yetu ari ya kuwalea watoto wetu huku tukitambua kuwa ni jukumu letu wazazi kuwaonyesha njia njema watoto wetu ili nao wapate kuyakabili maisha yao ya baadae katika hali stahiki.

 

Tunaomba hayo kwanjia ya Kristo bwana wetu amina

Kwa jina la baba na la mwana…

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu Sauti ya Faraja kutoka Kagera, kipindi kilichopita nilizungumzia juu ya aina ya wazazi wawajibikaji na moja kwa moja nikaelezea sifa za wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto. Nilisema wazazi wawajibikaji hutoa malezi yaliyo bora kwa watoto wao, tena nikasema kuwa wazazi wawajibikaji wanaifanya familia kuwa kanisa la nyumbani. Vilevile nilisema kuwa wazazi hawa wawajibikaji ni wale wanaoifanya familia kuwa shule ya nyumbani kwani hujitahidi kutoa mafunzo yote stahiki kimaadili kwa watoto wao. Sifa nyingine ya wazazi wawajibikaji niliyoeleza nilisema ni kutoa somo ama mafunzo ya utii kwa watoto wao. Tena nilieleza kuwa wazazi wawajibikaji wanawalea watoto wao kuwa waaminifu. Na nikasema sifa nyingine kwamba, wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto wao huwa wanatenga muda wa kukaa na watoto wao ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi stahiki. Halafu nikasema, Wanatimiza vema kazi yao wakijua kuwa wanatimiza kwa matendo sehemu ya viapo vyao vya ndoa; yaani kuwalea watoto wao kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake, huku wakiwarithisha watoto wao mila za wazee zilizo njema. (Rej. Mithali 19:18, Waefeso 6:4)

 

Wapendwa wasikilizaji, wa redio maria sauti ya kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake redio mbiu sauti ya faraja kutoka Kagera, ukiachana na hii aina ya wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto ambapo kwa hakika ndio aina niliyosema kuwa ndiyo inayopaswa kuigwa, leo napenda nifafanue aina kadhaa za wazazi ambazo nazo leo hii zipo kwenye jamii zetu ijapokuwa hazipaswi kuigwa kabisa. Kwa hakika aina hizi za wazazi ni chukivu kwa Mungu, kwa kanisa na kwa jamii yote kwani aina hizi zimeweza kuzalisha watu majambazi, wahuni, watu wakatili, walevi, wavivu, wapagani, wezi, wajuaji, watu walioathirika kisaikolojia, watoto wasiochukulika, maadui kwa wazazi wao, na kwa ujumla watoto wa tabia mbalimbali ambazo hazipaswi kuigwa hata kidogo kwenye jamii zetu.

Wapendwa wasikilizaji, aina mojawapo ya wazazi ambao ni chukivu ni ile ya wazazi ruksa. Hawa ni wazazi ambao kwakweli hawana sifa ya kuitwa wazazi zaidi ya sifa moja tu ya kuzaa ambayo walau inawaheshimisha. Kwa hakika, wazazi hawa kwanza wenyewe hawana maadili. Mara zote watoto wamekuwa ndio wa kuwaongoza ama kuwaendesha. Daima wazazi wa ruksa wamekuwa wakikubaliana na chochote kile wanachoambiwa na watoto wao. Ee, Mtoto akisema anatoka haulizwi anaenda wapi na wala kwamba huko anakoenda anaenda kufanya nini. Mtoto akisema amechoka na hivyo hataenda kanisani ama shuleni mzazi anasema sawa! Akimwona mwanae anapigana na mtoto wa jirani anashabikia na pengine na yeye kuongezea konzi pasipo kuzuia shari. Kila kitu wazazi hao wanaruhusuruhusu tu. Wazazi wa aina hii hawana neno hapana hata siku moja katika vinywani mwao. Ni wazazi ambao hawana misingi ya kimaadili na kwahiyo kwakuwa hawataki kufikiri zaidi, basi watoto wanawapanda vichwani na hivyo kuamua wanavyotaka siku zote.  Wazazi hawa wanashindwa kujua kuwa Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; watoto ni tuzo lake Mungu kwetu sisi. (Zaburi: 127:3) Ndugu zangu watoto waliotoka kwenye familia ya aina hii ya wazazi wenye kuruhusu kila kitu bila ya kuchuja mambo ni lazima maisha yawapige na wala sio kidogo kwani kwakuwa hawakuwahi kusikia neno acha ama hapana kutoka kwenye vinywa vya wazazi wao, wanakuwa wa ajabu kupindukia. Sina shaka msikilizaji wangu ulishawahi kukutana na wazazi wa aina hii.

 

Wapendwa wasikilizaji, ukiacha hawa wazazi ambao daima hawajui kukataa kitu chochote kutoka kwa watoto wao hata kama ni kibaya, kuna wazazi wengine leo hii ambao ni wazazi wakandamizaji wa watoto wao. Wazazi hawa ni wakatili sana kwa watoto wao. Wao wanachoamini ni kwamba mtoto hapaswi kuongea kitu na akasikilizwa. Wao wanajua tu kuwa njia sahihi ya kumlea mtoto ni kumpiga ama kumnyamazisha asitoe sauti, na hapo watakuwa wamekamilisha zoezi zima la malezi. Ee, unakuta mtoto anamwambia mama. mamaaa, au babaaa naomba… kabla hajamaliza sentensi mama au baba ameshamfokea, tuliaa weweee! Sitaki ujinga wako. Mtoto masikini anaondoka akiwa amenyong’onyea utamwonea huruma. Wazazi hawa siku zote iwe mtoto kafanya jambo jema ama jambo baya kwao ni mtindo mmoja. Hawana masahihisho kwa watoto wao kabisa. Mtoto akikosea kidogo tuu siku hiyo atavimba mwili kwa viboko ama vifinyo. Ama mtoto akijaribu kueleza kitu atanyamazishwa hata kabla ya mzazi kujua kuwa kitu hicho kina tija ama vipi. Tena sauti itakayotolewa na mzazi utadhani ni ile ya askari vitani. Na kama mtoto kiafya ni wale wembamba wembamba basi unaweza kumkuta yuko chini anajikongoja kuamka ajisikilizie. Ndugu zangu kwa hali ya wazazi wa aina hii, Ndio unakuta mtoto anapitia changamoto fulani kubwa tu kama vile masuala ya kikatili yanayowasibu watoto wetu ya ulawiti, ubakaji na au kama alikutana na mtu mwenye dalili ya kumteka! lakini kwakuwa anajua kuwa hatasikilizwa akijieleza, basi anaamua kujikalia na shida yake na mwisho wa siku inakuwa kubwa hata kumuathiri vibaya zaidi kuliko kama angesikilizwa na kusaidiwa mapema.

Ndugu zangu wasikilizaji, watoto waliozaliwa katika familia za tabia ama aina hii, huwa kwa asili wanakuwa watu waoga wasioweza kusimama mbele ya watu na kuongea, watu wasiojiamini kuwa wanaweza jambo, watu wenye maumivu ya ndani, watu wasiojua kupenda wala kupendwa, watu wayamafu, watu ambao daima wanakuwa na mawazo mengi kichwani. Kwa mfano kama unamuuliza kitu unaweza kuhisi amekunyamazia kumbe mwenzako hajakusikia, yupo mbaaaali. Na pengine wanakuwa watu wasiojua thamani ya mzazi katika maisha yao yote kwakuwa nao hawakuthaminiwa. Ni watu ambao nao wataweza kukitendea kizazi chao kama wao walivyotendewa. Na ndugu zangu watu hawa daima huwa wenye tabia nyingi za chinichini, watu wasio wawazi katika mipango yao na mienendo yao kwa ujumla, kwasababu katika maisha yao hawakupata mwanya wa kusikilizwa. Ndugu msikilizaji sina shaka ulishaona wazazi kama hawa katika jamii inayokuzunguka.

Ndugu zangu wasikilizaji, ukiachana na wazazi wa ruksa na wale wakandamizaji, kwenye jamii zetu pia kuna aina ya wazazi wazembe na watepetevu katika kuwalea watoto wao. Wazazi hawa ni wale waliokosa umakini kabisa katika kutelekeza wajibu wao kama wazazi. Wazazi wa aina hii ndugu zangu, hawajali wala hawajui ni yapi yanayowasibu watoto wao. Hata kama mtoto kaumia mzazi hawajibiki ipasavyo kuona ni kwa namna gani mtoto kaumia. Wazazi hawa daima wamekuwa na tabia ya kujisingizia kuwa wapo bize na shughuli tu. Wazazi wa aina hii hata ungewauliza hali za watoto wao, wao hawazijui vizuri! Hawazijui kwakuwa hawana hata muda wa kuwauliza kwamba wameshindaje, au wameamkaje au wanaendeleaje na masomo ama afya zao zikoje. Wazazi hawa watoto wao wakifeli masomo kwao ni sawa tu, wakibainika kuwa na tabia mbaya kimaadili, wao hawatilii shaka yoyote hata wakishtuliwa na wazazi wenzao. Hata wakisikia kuna huu udhalilishaji wa watoto ambao kwa siku hizi umepamba moto, wao huwa hawatilii maanani kwani kwakuwa ni wazembe, hawatakagi kusugua vichwa vyao kutafuta namna nzuri ya kuwalinda watoto wao. Kwasababu hii, hufika wakati kuona kwamba hawawafahamu watoto wao kabisa; hawajui vilio na furaha za wototo wao. Wao wamezama kabisa katika biashara na mambo mengineyo. Ndugu zangu wasikilizaji wazazi wa namna hii katika jamii ni sumu kabisa kwani hupotosha maadili ya watoto wao na hivyo kuathiri pia jamii inayowazunguka. Sina shaka kabisa kuwa na aina ya wazazi ruksa msikilizaji wangu umeshakumbana nayo na huenda ikakukera sana kwamba kwanini mambo yaende au yawe hivi!

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya Kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu Sauti ya Faraja kutoka mkoani Kagera, unayenisikiliza muda huu ni mimi Sista Anagladness Mrumah kutoka ofisi ya Mashirika ya Kipapa na katibu wa Utoto mtakatifu taifa, hapa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Utakumbuka kuwa kipindi kilichopita nilizungumzia juu ya sifa za wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto. Basi mwanzoni mwa kipindi hiki cha leo nimerudia kwa ufupi zile sifa za wazazi wawajibikaji na halafu nikaenda moja kwa moja kwenye aina za nyingine za wazazi ambao nao hawa wapo katika jamii zetu. Wazazi ambao kwakweli wamekuwa kero katika kudidimiza malezi kwa watoto wao na jamii kwa ujumla. Nimezungumza juu ya wazazi ambao wana tabia ya kuruhusu kila jambo kwa watoto wao bila kuchuja kuwa ni jema ama baya na kwahiyo kuwaweka watoto matatani kwa kukosa mielekeo. Tena nimezungumzia juu ya wazazi wakandamizaji yaani wazazi wakatili ambao kwa hakika wao wanadhani kuwa kumkoromea mtoto ama kumpiga ndio malezi sahihi, kumbe ni kumnyong’onyeza mtoto na hivyo kuathirika kisaikolojia au kumfanya awe wa kufanya mambo kichinichini ili kukwepa adhabu kwa kukosa uhuru. Na halafu nimeelezea juu ya wazazi wazembe katika kutoa malezi kwasababu tu ya ubize wao, jambo ambalo leo hii limezalisha kizazi kichanga ambacho hakijielewi kabisa. Hayo ndiyo niliyotangulia kuyazungumza. Karibu uendelee kunifuatilia.

Wapendwa wasikilizaji, kwenye jamii zetu wapo pia wazazi wapuuziaji wa mambo katika kutoa malezi kwa watoto. Yaani wao daima kila kitu huona kana kwamba hakina maana kumbe kina maana kubwa. Kila kitu kwao wanaona kuwa ni cha kuachilia mbali kwani hakiwahusu. Hata kama utamwambia mzazi wa namna hii kuwa mtoto wake akiaga kwamba anaenda shule huwa hafiki shuleni yeye atakwambia wanamzushia tu mwanangu hana tabia kama hiyo. Utaweza kumwambia kuwa mwanae ana tabia ya wizi halafu yeye akasema muache aibe akishikwa apigwe. Au utaweza kumwambia kuwa mtoto wake anajihusisha na mahusiano mabaya na yeye akakujibu kuwa wanamuonea mwanae, na mambo mengine kama hayo. Wazazi wa wapuuziaji wa mambo huwa na hulka ya kutokujali mambo wayaonayo kwa macho yao ama wanayoyasikia kwa watu wengine juu ya watoto wao. Wao huchukulia mambo kirahisirahisi tu. Hata wakisikia habari mbaya juu ya watoto wao, wao wanapuuzia au hata pengine kutetea upuuzi wa watoto wao. Hawaweki umakini wa kutosha katika habari wanazozisikia juu ya watoto wao. Matokeo yake kutokana na hali yao ya kupuuzia mambo, watoto wao wanawaozea mikononi mwao na inakuwa ni kero kwao wenyewe, kwa majirani, kero mashuleni kwao na kero kanisani. Unakuta mtu misa inaendelea yeye anachati. Ama mipango mikakati ya kuendeleza jumuiya ndogondogo, kigango, parokia ama jimbo inawekwa, lakini yeye anaona kuwa sio mpango wake wa kwanza kichwani mwake. Kumbe wazazi hawa wangekuwa makini na yale yasemwayo juu ya watoto wao, walao wangeweza kuwasaidia na kuwaunda katika utu wema.

Na tena wazazi wa aina hii huwa hawaoni aibu kuleta mfano mbaya kwa watoto wao. Watapigana mbele ya watoto, watatukanana mbele ya watoto, watadhalilishana, watafanya kila kufuru mbele za watoto. Watatenda matendo mabovu machoni pa watoto wao, wakisingizia eti ndiyo maisha ya kizungu. Si wana hulka ya kupuuzia mambo? Matokeo yake watoto wao nao wakifanya upuuzi wanakosa nguvu kabisa ya kuwanidhamisha kwasababu wanaona soni kuwa watawaambia kuwa na wao wanayafanya. Bila shaka na aina hii ya wazazi wapuuziaji wa mambo nayo ulishaishuhudia katika maisha yako mpendwa msikilizaji wangu!

Wapendwa wasikilizaji, kuna aina ya wazazi inayoitwa wazazi bubu. Wazazi bubu ndio basi tena. Kwenye familia zao hawana hulka ya kufundisha watoto, wala kuelekeza, au kuonya watoto, na wala kuwasahihisha wanapokosea. Wao wapo tu kama hawapo. Familia ya namna hii inakuwa na mporomoko mkubwa sana wa maadili; na ni hatari kubwa sana kwa majirani. Eti mzazi anaona akimsahihisha mwanae atakuwa anamwonea, Kweli? Wapendwa wasikilizaji, tusiwe wazazi bubu! La sivyo, tutajitengenezea wenyewe mabomu ndani ya familia zetu, ambapo siku yakilipuka yataanza na sisi wa karibu! Kutopenda kuongea chochote kinachohusu malezi ni kuwapa watoto fursa ya kuendelea na yao. Sasa kwakuwa mzazi ni dereva na watoto ni abiria, hebu dereva ahakikishe kuwa taratibu zote za safari zipo sawa, ili kusudi awafikishe abiria (ndio watoto wake) kwenye sehemu sahihi, watoto wasije wakachukua jukumu la kukupelekesha wewe mzazi usipopastahili. Eheeee, msikilizaji, hujawahi kuona ama kusikia wazazi bubu kwenye mazingira yako?

Aina nyingine wapendwa wasikilizaji ni ile ya wazazi wasinziaji. Hawa husinzia sana katika utendaji wao wa mambo. Wazazi hawa hawana ule wepesi wa kutatua matatizo ya familia zao kwa wakati mwafaka. Daima wao huacha mambo hadi yanaoza ndio wanakurupuka. Hata kama mtoto ameshaonyesha dalili za kuumwa, kwao si rahisi kuchukua tahadhari ya kwenda hospitali mtoto akachekiwe mapema na kisha kupata dawa. watasubiri kwanza weee, mpaka awe hoi ndipo pilika pilika za kumkimbiza ilipo hospitali huanza. Wao maamuzi hufanywa baada ya mambo kuanza kuharibika. Wanakuwa kama lile gari la zima moto ambalo kama hakuna moto huwa halina kazi, linaegeshwa mahali hadi hapo kutakapotokea dhara mahali. Ukija kwenye masuala ya shule, watoto ni lazima wayumbe. Wazazi wasinziaji Hawaandai malipo yanayohitajiwa shuleni kwa ajili ya watoto wao kama vile ada, matumizi binafsi ya watoto pamoja na michango mingine kwa wakati unaofaa. Matokeo yake watoto wao daima wanakuwa ni watu wa kuchelewa sana kwenda mashuleni au wanapofika mashuleni kurudishwa nyumbani wakalete mambo yanayohitajiwa ambayo kwa kusinzia kwa wazazi wao hawakufanikiwa kuja nayo. Katika mambo ya kanisa pia hawawajibiki kwa wakati mwafaka, muda wote wamezinzia wanaota ndoto za kimweri. Msikilizaji kama hujakutana na aina hii ya wazazi wasinziaji, ipo siku utakutana nayo kwani wapo wazazi wengi ambao ni wasinziaji kwenye kutekeleza jambo la kimalezi kwa wakati wake.

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya Kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu Sauti ya Faraja kutoka mkoani Kagera, Aina ya mwisho ni ile ya wazazi wenye hatia. aina hii ya wazazi inatokana na matokeo hasi ya aina hizi nyingine ambazo nimezijadili leo kama vile, wazazi ruksa, wazazi wakandamizaji, wazazi wazembe na watepetevu na wazazi wasinziaji. wazazi wenye hatia ni aina ya wazazi ambao wana majuto makubwa ambayo yanasababishwa na yale waliyokengeuka katika kutoa malezi kwa watoto wao. Kwa kifupi haya ni majuto wanayoyapata wazazi ambao walishindwa kuwajibika vyema kuwalea watoto wao. hujiona kuwa ni watu wenye hatia daima. Watoto wanapokuwa mbali, wazazi ambao hawakutimiza wajibu zao vema huona kama wanaadhibiwa kutokana na dhambi walizozifanya. Au hata kama watoto wao watawatunza vizuri, ile hali ya aibu kwamba kwa kweli sikuwatendea watoto wangu haki, nilimtesa sana mama yao, niliifilisi familia na sasa wao wananitunza; sijui wananifikiriaje’! au mama kama alishawahi kuacha ndoa na kurudi kwao na kuwaacha watoto wanayongayonga, akifikia uzeeni anaumwa na roho. Badala afurahie maisha kwasababu wanawe wana chochote kitu, kwake vinamsuta tu.  Na pengine anaweza akawaza kuwa hata hicho watoto wanachompatia huenda hawampi kingi cha kuridhisha kwakuwa aliwatesa. Daima anakuwa mtu wa kujilalamisha tu. Hata kama watoto wanawapatia wazazi wao nguo za kila aina baada ya kufanikiwa kimaisha ama kujaza kila kitu cha kula kizuri ndani, bado wazazi hawa hawataonekana kwamba wana kila kitu kwasababu ya kufinywa na dhamiri zao kwa ajili ya makosa waliyowafanyia watoto wao huko nyuma! Tafiti zinatuonesha kuwa wazazi wa namna hii hufa mapema sana na wanapokea kifo wakiwa na majonzi mengi sana. Bila shaka kati ya wasikilizaji wangi wa muda huu mmeshawahi kukutana na wazazi wenye hatia.

Wapendwa wasikilizaji, nihitimishe kipindi kwa kusema hiviiii, hebu jamani kila mzazi awe muwajibikaji katika kutoa malezi stahiki kwa watoto ama mtoto wake. katika shamba, mkulima huvuna mazao bora kama na kama tu aliweza kutunza mazao haya tangu aliposia mbegu hadi kufikia muda wa mavuno. Sasa na sisi, ikiwa tunatarajia kuwa na watoto ambao ni vijana na watu wazima wa baadaye wazuri, basi na tuwe tunahakikisha kwamba tunawalea kiaminifu sawasawa na matarajio yetu. Tusitarajie kuwa vitu vizuri vinapatikana katika ndoto za usiku, hapana, ndoto nyingine hata hazina uhalisia kabisa. Waweza kuwa usingizini na kuhisi umepata fedha nyingi sana za kutatua shida zako zote, au kumiliki kitu kizuri cha thamani lakini cha kushangaza asubuhi unaamkia patupu. Sasa na sisi wazazi wakati ndio sasa wa kuwalea watoto wetu wakingali wadogo, tena tuwalee tukiwa na malengo makubwa ya kuwafikisha sehemu nzuri kimaisha, ili baadae badala ya kuwa wazazi wenye simanzi, tuwe wazazi wanaofurahia uzao wao. Hima, kipindi cha kung’ang’ana na malezi ni hiki watoto wakingali wadogo, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Ukimkuza vizuri ni Baraka kwako na ukimlea tofauti, majuto yatakufuata.

 

 

Sr Anagladness Mrumah

Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa