Mtoto hujengwa kwanza na maneno anayoyasikia nyumbani
Katika safari ya malezi, wazazi wengi huzingatia mambo mengi muhimu kwa watoto wao: elimu bora, chakula, mavazi, afya na mazingira salama ya kukulia. Haya yote ni muhimu, lakini kuna eneo moja ambalo mara nyingi husahaulika, nalo ni nguvu ya maneno ambayo mtoto anayapokea kila siku kutoka kwa wazazi wake.
Kabla mtoto hajajifunza namna ya kuzungumza na dunia, hujifunza kwanza sauti ya nyumbani kwake. Kabla hajajua watu wengine watamthamini au kumkosoa vipi, tayari ameanza kujenga picha yake kupitia maneno anayoyasikia kutoka kwa wale anaowapenda zaidi.
Ndiyo maana katika mfululizo wa kipindi chetu cha “MTOTO NI MALEZI”, tunazungumzia mada muhimu:
“MANENO YA MZAZI NI MBEGU.”
Kwa sababu kila neno linalotoka kwa mzazi linaweza kuwa mbegu inayopandwa ndani ya moyo wa mtoto. Mbegu hiyo inaweza kuzaa ujasiri, matumaini, upendo na heshima; au inaweza kuzaa hofu, maumivu na kukata tamaa.
Mtoto hasikii maneno pekee, anajenga maisha kupitia maneno hayo
Mtoto mdogo anapozaliwa hana uwezo wa kujitathmini mwenyewe. Hajui uwezo wake, thamani yake wala nafasi yake katika dunia. Mara nyingi hujifunza mambo hayo kupitia namna wazazi wake wanavyomzungumzia.
Mzazi anayemwambia mtoto: “Unaweza kufanya vizuri.” “Ninaamini katika uwezo wako.” “Mungu amekuumba kwa kusudi.” anakuwa anajenga moyo wa mtoto kuwa na matumaini na kujiamini. Lakini mtoto anayesikia mara kwa mara maneno kama: “Wewe huwezi.” “Hutakuwa kitu.” “Kila siku ni tatizo kwako.” anaweza kuanza kuamini kwamba kweli hana uwezo au thamani. Hapa ndipo wazazi wanapaswa kuelewa kwamba maneno si sauti zinazopita na kutoweka. Baadhi ya maneno hubaki moyoni kwa muda mrefu sana. Mtoto anaweza kusahau zawadi aliyopewa, lakini mara nyingi hatasahau namna mzazi wake alivyomfanya ajisikie.
Biblia inatufundisha kuwa makini na ulimi wetu
Neno la Mungu linaweka wazi umuhimu wa maneno katika maisha ya mwanadamu.
Katika Mithali 18:21, Biblia inasema: “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; na wao waupendao watakula matunda yake.” Andiko hili linatufundisha kwamba maneno yana nguvu. Ulimi unaweza kujenga au kubomoa. Unaweza kuleta faraja au maumivu. Unaweza kumuinua mtu au kumkatisha tamaa. Kwa mzazi, ujumbe huu una uzito mkubwa zaidi kwa sababu mtoto ana nafasi ya kipekee katika kupokea maneno ya wazazi wake. Mtoto anahitaji kusikia maneno ya maelekezo, lakini pia anahitaji kusikia maneno ya upendo. Anahitaji kusahihishwa, lakini pia anahitaji kutiwa moyo. Anahitaji kuelekezwa, lakini pia anahitaji kuhakikishiwa kwamba bado ana thamani hata anapokosea.
Kumrekebisha mtoto si sawa na kumvunja moyo
Malezi bora hayamaanishi kumruhusu mtoto afanye kila kitu anachotaka. Mtoto anahitaji mipaka, maelekezo na nidhamu.
Lakini kuna tofauti kubwa kati ya kurekebisha tabia ya mtoto na kushambulia utu wa mtoto.
Mzazi mwenye hekima anaweza kusema: “Ulichofanya si sahihi, lakini unaweza kujifunza na kubadilika.”Badala ya kusema: “Wewe ni mtoto mbaya na hutabadilika.” Katika hali ya kwanza, mzazi anashughulikia kosa. Katika hali ya pili, mzazi anaweza kumfanya mtoto ajione yeye mwenyewe ndiye tatizo. Mtoto anaweza kufanya kosa, lakini kosa lake halipaswi kumfanya aamini kwamba yeye hana thamani. Malezi yenye upendo humsaidia mtoto kuona kwamba anaweza kubadilika na kuwa bora zaidi.
Nyumba ndiyo shule ya kwanza ya lugha
Kabla mtoto hajafika shuleni, tayari ameshaanza kupata masomo muhimu nyumbani. Huko anajifunza namna ya kuzungumza. Anajifunza namna ya kushughulikia matatizo. Anajifunza namna ya kuwaheshimu wengine. Anajifunza namna ya kuonyesha upendo. Mtoto anayekulia katika nyumba yenye maneno ya heshima hujifunza heshima. Mtoto anayekulia katika nyumba yenye msamaha hujifunza kusamehe. Mtoto anayekulia katika nyumba yenye shukrani hujifunza kuthamini. Kwa hiyo, mzazi anapobadilisha lugha yake nyumbani, anabadilisha pia mazingira ambayo mtoto anakulia.
Maneno ya mzazi ni sehemu ya urithi wa mtoto
Wazazi wengi hufikiria urithi wa mtoto ni mali, elimu au vitu watakavyomuachia. Haya ni mambo mazuri, lakini kuna urithi mwingine ambao una nguvu kubwa zaidi:
Maneno na misingi wanayoweka ndani ya moyo wa mtoto.
Mtoto anayekua akisikia maneno ya hekima, maombi na matumaini hubeba urithi huo maisha yake yote. Siku moja mtoto atakua na kuondoka nyumbani. Huenda asibebe kila kitu ulichomnulia, lakini atabeba kile ulichomjengea ndani yake. Atabeba namna ulivyomfundisha kujiona. Atabeba namna ulivyomfundisha kuwaheshimu wengine. Atabeba namna ulivyomwelekeza kwa Mungu.
Mzazi, chagua maneno yatakayobeba baraka
Kila siku mzazi anapata nafasi ya kupanda mbegu ndani ya mtoto wake. Unaweza kupanda mbegu ya hofu au ujasiri. Unaweza kupanda mbegu ya kukata tamaa au matumaini. Unaweza kupanda mbegu ya maumivu au uponyaji. Chagua maneno yatakayomjenga mtoto wako, Mfundishe, Mrekebishe na Muongoze.
Lakini daima mkumbushe kwamba anapendwa na ana thamani mbele za Mungu. Biblia inasema katika Waefeso 4:29: “Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wasikiao.” Huu ni mwaliko kwa kila mzazi kulinda maneno yake, kwa sababu maneno hayo yanaweza kuwa chanzo cha nguvu katika maisha ya mtoto.
Hitimisho
“MTOTO NI MALEZI” inatukumbusha kwamba watoto hawajengwi kwa mahitaji wanayopewa pekee, bali kwa upendo, mfano na maneno wanayosikia kila siku. Mzazi mpendwa, mtoto wako anasikia zaidi ya unavyofikiri. Anakumbuka zaidi ya unavyodhani. Na maneno yako yana nguvu zaidi ya unavyoweza kuona. Kwa hiyo, kabla hujazungumza, kumbuka:
Maneno ya mzazi ni mbegu.
Panda mbegu nzuri leo, ili kesho uvune mtoto mwenye heshima, ujasiri, upendo na hofu ya Mungu.

 

 

Imeandaliwa na Sr. Anagladness Mrumah: Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa