Posts by adminpmstec2020

KONGAMANO LA UTOTO MTAKATIFU PAROKIA YA LUNDUMATO , 20-24 AGOSTI, 2025

Watoto wa 402 wa Parokia ya Lundumato walifanya kongamano la kiparokia, kuanzia tarehe 20-24 Agosti, 2025. Kwa muda wote wa Kongamano watoto walikuwa kupata semina mbalimbali za kuwajenga kiroho na kimaadili. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tarehe 23 siku ya Jumamosi, watoto waliweza kujiunga na kanisa la Tanzania kwa lengo la kuombea Haki na Amani vitawale, hasa katika uchaguzi mkuu wa viongozi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu. Kwahiyo, Pamoja na nia hiyo muhimu, walifundishwa mada 2 ambazo ni, Historia ya Shirika la Kipapa na Muundo wake na Maisha ya Wito na Sala.

Kwa kutambua kuwa walezi ni nguzo katika kusimama na kukua kwa shirika hili, walifundishwa mada ya Ulinzi wa mtoto ili wapate ujuzi wa kuwalinda watoto katika utume wao wa kulea. Idadi ya watoto walioshiriki kongamano ni 402.

Jumamosi usiku tulikuwa na Saa Takatifu tukiabudu Ekaristi kuamkia Dominika ambayo kongamano lilihitimishwa kwa Misa Takatifu kuombea Haki na Amani.

 

 

 

Imetayarishwa na Pd. Erasto Nyimbo, Mkurugenzi PMS Jimbo

Read more

SIFA ZA AINA YA WAZAZI WASIOFAA KUIGWA KATIKA KUTOA MALEZI KWA WATOTO

Kwajina la Baba na la Mwana naa Roho Mtakatifu …

Bwana Yesu tunakushukuru kwa baraka zako unazotujalia siku hata siku. Tunaomba uendelee kuichochea mioyo yetu ari ya kuwalea watoto wetu huku tukitambua kuwa ni jukumu letu wazazi kuwaonyesha njia njema watoto wetu ili nao wapate kuyakabili maisha yao ya baadae katika hali stahiki.

 

Tunaomba hayo kwanjia ya Kristo bwana wetu amina

Kwa jina la baba na la mwana…

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu Sauti ya Faraja kutoka Kagera, kipindi kilichopita nilizungumzia juu ya aina ya wazazi wawajibikaji na moja kwa moja nikaelezea sifa za wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto. Nilisema wazazi wawajibikaji hutoa malezi yaliyo bora kwa watoto wao, tena nikasema kuwa wazazi wawajibikaji wanaifanya familia kuwa kanisa la nyumbani. Vilevile nilisema kuwa wazazi hawa wawajibikaji ni wale wanaoifanya familia kuwa shule ya nyumbani kwani hujitahidi kutoa mafunzo yote stahiki kimaadili kwa watoto wao. Sifa nyingine ya wazazi wawajibikaji niliyoeleza nilisema ni kutoa somo ama mafunzo ya utii kwa watoto wao. Tena nilieleza kuwa wazazi wawajibikaji wanawalea watoto wao kuwa waaminifu. Na nikasema sifa nyingine kwamba, wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto wao huwa wanatenga muda wa kukaa na watoto wao ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi stahiki. Halafu nikasema, Wanatimiza vema kazi yao wakijua kuwa wanatimiza kwa matendo sehemu ya viapo vyao vya ndoa; yaani kuwalea watoto wao kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake, huku wakiwarithisha watoto wao mila za wazee zilizo njema. (Rej. Mithali 19:18, Waefeso 6:4)

 

Wapendwa wasikilizaji, wa redio maria sauti ya kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake redio mbiu sauti ya faraja kutoka Kagera, ukiachana na hii aina ya wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto ambapo kwa hakika ndio aina niliyosema kuwa ndiyo inayopaswa kuigwa, leo napenda nifafanue aina kadhaa za wazazi ambazo nazo leo hii zipo kwenye jamii zetu ijapokuwa hazipaswi kuigwa kabisa. Kwa hakika aina hizi za wazazi ni chukivu kwa Mungu, kwa kanisa na kwa jamii yote kwani aina hizi zimeweza kuzalisha watu majambazi, wahuni, watu wakatili, walevi, wavivu, wapagani, wezi, wajuaji, watu walioathirika kisaikolojia, watoto wasiochukulika, maadui kwa wazazi wao, na kwa ujumla watoto wa tabia mbalimbali ambazo hazipaswi kuigwa hata kidogo kwenye jamii zetu.

Wapendwa wasikilizaji, aina mojawapo ya wazazi ambao ni chukivu ni ile ya wazazi ruksa. Hawa ni wazazi ambao kwakweli hawana sifa ya kuitwa wazazi zaidi ya sifa moja tu ya kuzaa ambayo walau inawaheshimisha. Kwa hakika, wazazi hawa kwanza wenyewe hawana maadili. Mara zote watoto wamekuwa ndio wa kuwaongoza ama kuwaendesha. Daima wazazi wa ruksa wamekuwa wakikubaliana na chochote kile wanachoambiwa na watoto wao. Ee, Mtoto akisema anatoka haulizwi anaenda wapi na wala kwamba huko anakoenda anaenda kufanya nini. Mtoto akisema amechoka na hivyo hataenda kanisani ama shuleni mzazi anasema sawa! Akimwona mwanae anapigana na mtoto wa jirani anashabikia na pengine na yeye kuongezea konzi pasipo kuzuia shari. Kila kitu wazazi hao wanaruhusuruhusu tu. Wazazi wa aina hii hawana neno hapana hata siku moja katika vinywani mwao. Ni wazazi ambao hawana misingi ya kimaadili na kwahiyo kwakuwa hawataki kufikiri zaidi, basi watoto wanawapanda vichwani na hivyo kuamua wanavyotaka siku zote.  Wazazi hawa wanashindwa kujua kuwa Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; watoto ni tuzo lake Mungu kwetu sisi. (Zaburi: 127:3) Ndugu zangu watoto waliotoka kwenye familia ya aina hii ya wazazi wenye kuruhusu kila kitu bila ya kuchuja mambo ni lazima maisha yawapige na wala sio kidogo kwani kwakuwa hawakuwahi kusikia neno acha ama hapana kutoka kwenye vinywa vya wazazi wao, wanakuwa wa ajabu kupindukia. Sina shaka msikilizaji wangu ulishawahi kukutana na wazazi wa aina hii.

 

Wapendwa wasikilizaji, ukiacha hawa wazazi ambao daima hawajui kukataa kitu chochote kutoka kwa watoto wao hata kama ni kibaya, kuna wazazi wengine leo hii ambao ni wazazi wakandamizaji wa watoto wao. Wazazi hawa ni wakatili sana kwa watoto wao. Wao wanachoamini ni kwamba mtoto hapaswi kuongea kitu na akasikilizwa. Wao wanajua tu kuwa njia sahihi ya kumlea mtoto ni kumpiga ama kumnyamazisha asitoe sauti, na hapo watakuwa wamekamilisha zoezi zima la malezi. Ee, unakuta mtoto anamwambia mama. mamaaa, au babaaa naomba… kabla hajamaliza sentensi mama au baba ameshamfokea, tuliaa weweee! Sitaki ujinga wako. Mtoto masikini anaondoka akiwa amenyong’onyea utamwonea huruma. Wazazi hawa siku zote iwe mtoto kafanya jambo jema ama jambo baya kwao ni mtindo mmoja. Hawana masahihisho kwa watoto wao kabisa. Mtoto akikosea kidogo tuu siku hiyo atavimba mwili kwa viboko ama vifinyo. Ama mtoto akijaribu kueleza kitu atanyamazishwa hata kabla ya mzazi kujua kuwa kitu hicho kina tija ama vipi. Tena sauti itakayotolewa na mzazi utadhani ni ile ya askari vitani. Na kama mtoto kiafya ni wale wembamba wembamba basi unaweza kumkuta yuko chini anajikongoja kuamka ajisikilizie. Ndugu zangu kwa hali ya wazazi wa aina hii, Ndio unakuta mtoto anapitia changamoto fulani kubwa tu kama vile masuala ya kikatili yanayowasibu watoto wetu ya ulawiti, ubakaji na au kama alikutana na mtu mwenye dalili ya kumteka! lakini kwakuwa anajua kuwa hatasikilizwa akijieleza, basi anaamua kujikalia na shida yake na mwisho wa siku inakuwa kubwa hata kumuathiri vibaya zaidi kuliko kama angesikilizwa na kusaidiwa mapema.

Ndugu zangu wasikilizaji, watoto waliozaliwa katika familia za tabia ama aina hii, huwa kwa asili wanakuwa watu waoga wasioweza kusimama mbele ya watu na kuongea, watu wasiojiamini kuwa wanaweza jambo, watu wenye maumivu ya ndani, watu wasiojua kupenda wala kupendwa, watu wayamafu, watu ambao daima wanakuwa na mawazo mengi kichwani. Kwa mfano kama unamuuliza kitu unaweza kuhisi amekunyamazia kumbe mwenzako hajakusikia, yupo mbaaaali. Na pengine wanakuwa watu wasiojua thamani ya mzazi katika maisha yao yote kwakuwa nao hawakuthaminiwa. Ni watu ambao nao wataweza kukitendea kizazi chao kama wao walivyotendewa. Na ndugu zangu watu hawa daima huwa wenye tabia nyingi za chinichini, watu wasio wawazi katika mipango yao na mienendo yao kwa ujumla, kwasababu katika maisha yao hawakupata mwanya wa kusikilizwa. Ndugu msikilizaji sina shaka ulishaona wazazi kama hawa katika jamii inayokuzunguka.

Ndugu zangu wasikilizaji, ukiachana na wazazi wa ruksa na wale wakandamizaji, kwenye jamii zetu pia kuna aina ya wazazi wazembe na watepetevu katika kuwalea watoto wao. Wazazi hawa ni wale waliokosa umakini kabisa katika kutelekeza wajibu wao kama wazazi. Wazazi wa aina hii ndugu zangu, hawajali wala hawajui ni yapi yanayowasibu watoto wao. Hata kama mtoto kaumia mzazi hawajibiki ipasavyo kuona ni kwa namna gani mtoto kaumia. Wazazi hawa daima wamekuwa na tabia ya kujisingizia kuwa wapo bize na shughuli tu. Wazazi wa aina hii hata ungewauliza hali za watoto wao, wao hawazijui vizuri! Hawazijui kwakuwa hawana hata muda wa kuwauliza kwamba wameshindaje, au wameamkaje au wanaendeleaje na masomo ama afya zao zikoje. Wazazi hawa watoto wao wakifeli masomo kwao ni sawa tu, wakibainika kuwa na tabia mbaya kimaadili, wao hawatilii shaka yoyote hata wakishtuliwa na wazazi wenzao. Hata wakisikia kuna huu udhalilishaji wa watoto ambao kwa siku hizi umepamba moto, wao huwa hawatilii maanani kwani kwakuwa ni wazembe, hawatakagi kusugua vichwa vyao kutafuta namna nzuri ya kuwalinda watoto wao. Kwasababu hii, hufika wakati kuona kwamba hawawafahamu watoto wao kabisa; hawajui vilio na furaha za wototo wao. Wao wamezama kabisa katika biashara na mambo mengineyo. Ndugu zangu wasikilizaji wazazi wa namna hii katika jamii ni sumu kabisa kwani hupotosha maadili ya watoto wao na hivyo kuathiri pia jamii inayowazunguka. Sina shaka kabisa kuwa na aina ya wazazi ruksa msikilizaji wangu umeshakumbana nayo na huenda ikakukera sana kwamba kwanini mambo yaende au yawe hivi!

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya Kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu Sauti ya Faraja kutoka mkoani Kagera, unayenisikiliza muda huu ni mimi Sista Anagladness Mrumah kutoka ofisi ya Mashirika ya Kipapa na katibu wa Utoto mtakatifu taifa, hapa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Utakumbuka kuwa kipindi kilichopita nilizungumzia juu ya sifa za wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto. Basi mwanzoni mwa kipindi hiki cha leo nimerudia kwa ufupi zile sifa za wazazi wawajibikaji na halafu nikaenda moja kwa moja kwenye aina za nyingine za wazazi ambao nao hawa wapo katika jamii zetu. Wazazi ambao kwakweli wamekuwa kero katika kudidimiza malezi kwa watoto wao na jamii kwa ujumla. Nimezungumza juu ya wazazi ambao wana tabia ya kuruhusu kila jambo kwa watoto wao bila kuchuja kuwa ni jema ama baya na kwahiyo kuwaweka watoto matatani kwa kukosa mielekeo. Tena nimezungumzia juu ya wazazi wakandamizaji yaani wazazi wakatili ambao kwa hakika wao wanadhani kuwa kumkoromea mtoto ama kumpiga ndio malezi sahihi, kumbe ni kumnyong’onyeza mtoto na hivyo kuathirika kisaikolojia au kumfanya awe wa kufanya mambo kichinichini ili kukwepa adhabu kwa kukosa uhuru. Na halafu nimeelezea juu ya wazazi wazembe katika kutoa malezi kwasababu tu ya ubize wao, jambo ambalo leo hii limezalisha kizazi kichanga ambacho hakijielewi kabisa. Hayo ndiyo niliyotangulia kuyazungumza. Karibu uendelee kunifuatilia.

Wapendwa wasikilizaji, kwenye jamii zetu wapo pia wazazi wapuuziaji wa mambo katika kutoa malezi kwa watoto. Yaani wao daima kila kitu huona kana kwamba hakina maana kumbe kina maana kubwa. Kila kitu kwao wanaona kuwa ni cha kuachilia mbali kwani hakiwahusu. Hata kama utamwambia mzazi wa namna hii kuwa mtoto wake akiaga kwamba anaenda shule huwa hafiki shuleni yeye atakwambia wanamzushia tu mwanangu hana tabia kama hiyo. Utaweza kumwambia kuwa mwanae ana tabia ya wizi halafu yeye akasema muache aibe akishikwa apigwe. Au utaweza kumwambia kuwa mtoto wake anajihusisha na mahusiano mabaya na yeye akakujibu kuwa wanamuonea mwanae, na mambo mengine kama hayo. Wazazi wa wapuuziaji wa mambo huwa na hulka ya kutokujali mambo wayaonayo kwa macho yao ama wanayoyasikia kwa watu wengine juu ya watoto wao. Wao huchukulia mambo kirahisirahisi tu. Hata wakisikia habari mbaya juu ya watoto wao, wao wanapuuzia au hata pengine kutetea upuuzi wa watoto wao. Hawaweki umakini wa kutosha katika habari wanazozisikia juu ya watoto wao. Matokeo yake kutokana na hali yao ya kupuuzia mambo, watoto wao wanawaozea mikononi mwao na inakuwa ni kero kwao wenyewe, kwa majirani, kero mashuleni kwao na kero kanisani. Unakuta mtu misa inaendelea yeye anachati. Ama mipango mikakati ya kuendeleza jumuiya ndogondogo, kigango, parokia ama jimbo inawekwa, lakini yeye anaona kuwa sio mpango wake wa kwanza kichwani mwake. Kumbe wazazi hawa wangekuwa makini na yale yasemwayo juu ya watoto wao, walao wangeweza kuwasaidia na kuwaunda katika utu wema.

Na tena wazazi wa aina hii huwa hawaoni aibu kuleta mfano mbaya kwa watoto wao. Watapigana mbele ya watoto, watatukanana mbele ya watoto, watadhalilishana, watafanya kila kufuru mbele za watoto. Watatenda matendo mabovu machoni pa watoto wao, wakisingizia eti ndiyo maisha ya kizungu. Si wana hulka ya kupuuzia mambo? Matokeo yake watoto wao nao wakifanya upuuzi wanakosa nguvu kabisa ya kuwanidhamisha kwasababu wanaona soni kuwa watawaambia kuwa na wao wanayafanya. Bila shaka na aina hii ya wazazi wapuuziaji wa mambo nayo ulishaishuhudia katika maisha yako mpendwa msikilizaji wangu!

Wapendwa wasikilizaji, kuna aina ya wazazi inayoitwa wazazi bubu. Wazazi bubu ndio basi tena. Kwenye familia zao hawana hulka ya kufundisha watoto, wala kuelekeza, au kuonya watoto, na wala kuwasahihisha wanapokosea. Wao wapo tu kama hawapo. Familia ya namna hii inakuwa na mporomoko mkubwa sana wa maadili; na ni hatari kubwa sana kwa majirani. Eti mzazi anaona akimsahihisha mwanae atakuwa anamwonea, Kweli? Wapendwa wasikilizaji, tusiwe wazazi bubu! La sivyo, tutajitengenezea wenyewe mabomu ndani ya familia zetu, ambapo siku yakilipuka yataanza na sisi wa karibu! Kutopenda kuongea chochote kinachohusu malezi ni kuwapa watoto fursa ya kuendelea na yao. Sasa kwakuwa mzazi ni dereva na watoto ni abiria, hebu dereva ahakikishe kuwa taratibu zote za safari zipo sawa, ili kusudi awafikishe abiria (ndio watoto wake) kwenye sehemu sahihi, watoto wasije wakachukua jukumu la kukupelekesha wewe mzazi usipopastahili. Eheeee, msikilizaji, hujawahi kuona ama kusikia wazazi bubu kwenye mazingira yako?

Aina nyingine wapendwa wasikilizaji ni ile ya wazazi wasinziaji. Hawa husinzia sana katika utendaji wao wa mambo. Wazazi hawa hawana ule wepesi wa kutatua matatizo ya familia zao kwa wakati mwafaka. Daima wao huacha mambo hadi yanaoza ndio wanakurupuka. Hata kama mtoto ameshaonyesha dalili za kuumwa, kwao si rahisi kuchukua tahadhari ya kwenda hospitali mtoto akachekiwe mapema na kisha kupata dawa. watasubiri kwanza weee, mpaka awe hoi ndipo pilika pilika za kumkimbiza ilipo hospitali huanza. Wao maamuzi hufanywa baada ya mambo kuanza kuharibika. Wanakuwa kama lile gari la zima moto ambalo kama hakuna moto huwa halina kazi, linaegeshwa mahali hadi hapo kutakapotokea dhara mahali. Ukija kwenye masuala ya shule, watoto ni lazima wayumbe. Wazazi wasinziaji Hawaandai malipo yanayohitajiwa shuleni kwa ajili ya watoto wao kama vile ada, matumizi binafsi ya watoto pamoja na michango mingine kwa wakati unaofaa. Matokeo yake watoto wao daima wanakuwa ni watu wa kuchelewa sana kwenda mashuleni au wanapofika mashuleni kurudishwa nyumbani wakalete mambo yanayohitajiwa ambayo kwa kusinzia kwa wazazi wao hawakufanikiwa kuja nayo. Katika mambo ya kanisa pia hawawajibiki kwa wakati mwafaka, muda wote wamezinzia wanaota ndoto za kimweri. Msikilizaji kama hujakutana na aina hii ya wazazi wasinziaji, ipo siku utakutana nayo kwani wapo wazazi wengi ambao ni wasinziaji kwenye kutekeleza jambo la kimalezi kwa wakati wake.

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya Kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu Sauti ya Faraja kutoka mkoani Kagera, Aina ya mwisho ni ile ya wazazi wenye hatia. aina hii ya wazazi inatokana na matokeo hasi ya aina hizi nyingine ambazo nimezijadili leo kama vile, wazazi ruksa, wazazi wakandamizaji, wazazi wazembe na watepetevu na wazazi wasinziaji. wazazi wenye hatia ni aina ya wazazi ambao wana majuto makubwa ambayo yanasababishwa na yale waliyokengeuka katika kutoa malezi kwa watoto wao. Kwa kifupi haya ni majuto wanayoyapata wazazi ambao walishindwa kuwajibika vyema kuwalea watoto wao. hujiona kuwa ni watu wenye hatia daima. Watoto wanapokuwa mbali, wazazi ambao hawakutimiza wajibu zao vema huona kama wanaadhibiwa kutokana na dhambi walizozifanya. Au hata kama watoto wao watawatunza vizuri, ile hali ya aibu kwamba kwa kweli sikuwatendea watoto wangu haki, nilimtesa sana mama yao, niliifilisi familia na sasa wao wananitunza; sijui wananifikiriaje’! au mama kama alishawahi kuacha ndoa na kurudi kwao na kuwaacha watoto wanayongayonga, akifikia uzeeni anaumwa na roho. Badala afurahie maisha kwasababu wanawe wana chochote kitu, kwake vinamsuta tu.  Na pengine anaweza akawaza kuwa hata hicho watoto wanachompatia huenda hawampi kingi cha kuridhisha kwakuwa aliwatesa. Daima anakuwa mtu wa kujilalamisha tu. Hata kama watoto wanawapatia wazazi wao nguo za kila aina baada ya kufanikiwa kimaisha ama kujaza kila kitu cha kula kizuri ndani, bado wazazi hawa hawataonekana kwamba wana kila kitu kwasababu ya kufinywa na dhamiri zao kwa ajili ya makosa waliyowafanyia watoto wao huko nyuma! Tafiti zinatuonesha kuwa wazazi wa namna hii hufa mapema sana na wanapokea kifo wakiwa na majonzi mengi sana. Bila shaka kati ya wasikilizaji wangi wa muda huu mmeshawahi kukutana na wazazi wenye hatia.

Wapendwa wasikilizaji, nihitimishe kipindi kwa kusema hiviiii, hebu jamani kila mzazi awe muwajibikaji katika kutoa malezi stahiki kwa watoto ama mtoto wake. katika shamba, mkulima huvuna mazao bora kama na kama tu aliweza kutunza mazao haya tangu aliposia mbegu hadi kufikia muda wa mavuno. Sasa na sisi, ikiwa tunatarajia kuwa na watoto ambao ni vijana na watu wazima wa baadaye wazuri, basi na tuwe tunahakikisha kwamba tunawalea kiaminifu sawasawa na matarajio yetu. Tusitarajie kuwa vitu vizuri vinapatikana katika ndoto za usiku, hapana, ndoto nyingine hata hazina uhalisia kabisa. Waweza kuwa usingizini na kuhisi umepata fedha nyingi sana za kutatua shida zako zote, au kumiliki kitu kizuri cha thamani lakini cha kushangaza asubuhi unaamkia patupu. Sasa na sisi wazazi wakati ndio sasa wa kuwalea watoto wetu wakingali wadogo, tena tuwalee tukiwa na malengo makubwa ya kuwafikisha sehemu nzuri kimaisha, ili baadae badala ya kuwa wazazi wenye simanzi, tuwe wazazi wanaofurahia uzao wao. Hima, kipindi cha kung’ang’ana na malezi ni hiki watoto wakingali wadogo, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Ukimkuza vizuri ni Baraka kwako na ukimlea tofauti, majuto yatakufuata.

 

 

Sr Anagladness Mrumah

Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa

 

 

 

 

Read more

MISSIONARY TRIP OF PMS NATIONAL DIRECTOR – ARCHDIOCESE OF MBEYA

On July 12th 2025, the PMS National Director Fr. Alfred Kwene, made a missionary trip to the Archdiocese of Mbeya, with the aim of meeting the PMS Diocesan leadership which is under the leadership of Fr Exavery Mwaifimbo. In addition, in this visit, the specific objective was to encourage the leaders for the good missionary work they do day by day. It was during these days; the Mbeya PMS Office was able to share with the National PMS Director their strategic plans that they have set for themselves in achieving their mission in that diocese.

 

 

 

Prepared by: Fr. Exavery, PMS Diocesan Director

Read more

MISA YA SHUKRANI BAADA YA MAADHIMISHO YA KONGAMANO LA UTOTO MTAKATIFU KANDA YA DSM (JIMBO KUU LA DSM)

Leo tarehe 8 Aprili, 2025 Utoto mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam waliadhimisha misa ya shukrani baada ya kumaliza Kongamano la Kanda ya Mashariki ambalo mwaka huu lilifanyika jimboni DSM kuanzia tarehe 19 –23 Juni, 2025 katika Parokia ya Kristo Mfalme Tabata. Katika kongamano hilo la kikanda, washiriki watoto kutoka majimbo saba (Jimbo kuu la DSM, Jimbo la Bagamoyo, Zanzibar, Tanga, Morogoro, Ifakara na Mahenge), walikuwa takribani 2600.

Misa ya shukrani kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo muhimu ilifanyika katika parokia ya Mt. Peter Clavery – Mbezi Louis. Mwazimishaji wa ibada ya misa takatifu alikuwa ni Padre Denis Agness Wigira, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika homilia yake Pd. Wigira aliwapongeza watoto pamoja na walezi kwa kuchukulia siku hii muhimu kwao kwani shukrani ni jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Hivyo aliwaasa waendelee kuona fahari katika hilo pamoja na kufurahia utume wao wa kimisionari siku zote. Misa hii ilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mashirika ya Kipapa (Sr Anagladness Mrumah, Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa pamoja na Sr Idda John Mketi ambaye ni katibu Muhtasi wa ofisi ya Mashirika ya Kipapa) ili kushirikiana na wanajimbo katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa makuu yake aliyowatendea.

 

 

 

Imeandaliwa na Sr Anagladness Mrumah, Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa

Read more

KONGAMANO LA UTOTO MTAKATIFU KANDA YA ZIWA VIKTORIA (19-23 JUNI, 2025)

Tarehe 19-22 Juni  tuliadhimisha Kongamano ya Kanda la Mwanza/Ziwa Victoria kwa ajili ya kuadhimisha mwaka wa Jubilei 2025 kwa ajili ya kuimarisha Imani ya Watoto wa Mashirika za Kipapa Kanda ya ziwa.  Yafuatayo ni majimbo ya kanda ya mwanza: Jimbo kuu la Mwanza, Musoma, Bunda, Shyinyanga, Geita, Rulenge-Ngara, Kayanga na Jimbo la Bukoba.

Bukoba watoto 546,  walezi 45, watawa 9,mapadre 2.  Shinyanga watoto 181 walezi 9 watawa 4 padre 1.  Musoma watoto 450 walezi 37 watawa 8. Bunda watoto 583, walezi 60,watawa 2, mapadre 1.Kayanga watoto 488walezi 26watawa 9 mapadre 1. Rulenge ngara  watoto 515, walezi 25, watawa 5. Geita watoto 70 walezi 47, watawa 2, mapadre 1. Mwanza watoto 835 walezi 62 watawa 10, mapadre 2

Kutoka majimbo haya tajwa hapo juu walihudhuria na kufurahia Kongamano hilo wakisema :”heri ingeendelea hadi wiki nzima”. Waliahidi awamu ijayo wataudhuria wengi zaidi.

Waliudhuria watawa  toka Mashirika mbalimbali wanaofanya utume wa kuwalea watoto kiimani na kimaadili.

Watoto walipata mada mbalimbali kutoka kwa watu mbalimbali kwamfano: Askofu wa Jimbo la Bukoba Jovitus Mwijage alifundisha mada :”Watoto waige maisha ya watakatifu. Mapadri wakurugenzi pia walitoa Mada kwa kukusisitiza watoto waendelee kujitambua Watoto walifurahia Mada zilizotolewa, michezo mbalimbali, burudani na nyimbo za utamaduni.

Misa ya ufunguzi iliadhimishwa na Askofu wa Bukoba, Jovinus Mwijage na Misa ya hitimisho iliadhimishwa na Askofu wa Jimbo la Geita Kasala, Flavian Kassala.

Michezo ya maswali na majibu kuhusu sakramenti, liturujia, historia ya kanisa

Michezo ya mpira kati ya mashabiki  wa yanga 3-1 Simba na michezo mingine ilichezwa katika kongamano hilo.

Kongamano la Kanda Limetusaidia Yafuatayo :

Watoto kusafiri kugundua mazingira mapya.

Watoto kujifunza kupitia Mada, michezo, burudani.

Watoto walijifunza kuishi mbali na familia kwa kujitegemea.

Tunamshukuru Mungu kutuwezesha kuadhimisha Kongamano na kumaliza Salama.

Tunamshukuru Rais wa PMS, askofu Jovitus Mwijage wa Jimbo la Bukoba kwa kutulisha neno, Mada  na kuhudhuria Kongamano. Tunamshukuru baba Mheshimiwa Mkurugenzi waTaifa PMS Padre Alfred Kwene kwa ushiriki wake. Aidha, tunawashukuru wakurugenzi wa majimbo yote ya Kanda ya kwa kushiriki wao mzuri. Shukran nyingi ziwaendee walezi na watoto kwa kuitikia na kuja katika kongamano hili.

 

Imeandaliwa na: Pd. Yvon, Mkurugenzi msaidizi wa PMS, Jimbo Kuu la Mwnza.

Read more

SIFA ZA WAZAZI WAWAJIBIKAJI KATIKA KUTOA MALEZI KWA WATOTO

Kwa jina la baba na la mwana na la roho mtakatifu Amina

Atukuzwe baba na mwana na roho mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote na milele amina

Bikira Maria Malkia wa familia, utuombee

Kwa jina la baba…………………..

Wapendwa wasikilizaji, hewani ni mimi Sr. Anagladness Mrumah wa shirika la Masista wa Usambara (COLU). Mimi ni katibu mtendaji wa Utoto Mtakatifu taifa, katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Karibu uu ngane name tangu mwanzo hadi mwisho wa kipindi hiki.

Mada ya leo ni kuhusu sifa za wazazi wawajibikaji

Ndugu zangu wasikilizaji, ni dhahiri katika jamii zetu malezi yamekuwa kila mara yanatofautiana kutoka mtoto mmoja na mwingine, kwasababu ya wahusika wakuu yaani wazazi ambao wapo katika aina tofauti tofauti. Kwa ajili ya hali hii, kwenye jamii kumekuwa na watoto wanaofaidi malezi thabiti kwa wazazi wao, wengine wakiwa wanapokea malezi vuguvugu, huku wengine kukosa malezi kabisa kutoka kwa wazazi wao, ambao wameonekana kuwa na mitazamo tofauti kwenye malezi.

Ndio maana mara nyingi wewe na mimi pengine tunajiuliza, ni kwanini mtoto huyu ana tabia hii, mwingine ile.  Kumbe ni kwasababu ya namna wazazi wanavyojiweka mbele ya watoto wao. Kwamfano, ukikuta mzazi ni muwajibikaji, basi watoto watapata malezi stahiki, mzazi akiwa ni yule wa kuruhusu kila kitu kiende katika familia, basi utakuta watoto nao wanateketea, ukikutana na wazazi wanaowakandamiza watoto kwenye familia, basi ujue hapa utakutana na watoto walioathirika kisaikolojia. Na kwenye familia nyingine kama utakutana na wazazi wazembe na watepetevu basi ujue malezi ya watoto wao yanakuwa na hali mbaya. Wazazi wengine kama watakuwa wapuuziaji wa mambo ujue kila kitu kitaenda kombo kwa watoto. Na kama wazazi wengine ni wale wasinziaji, ndio basi tena, kwenye jamii utakutana na watoto wasio na mwelekeo. Ndugu zangu hizi zote ni aina za wazazi ambao wanaishi katika jamii zetu yaani:

  • Wazazi wawajibikaji
  • Wazazi wa ruksa
  • Wazazi wakandamizaji
  • Wazazi wazembe na watepetevu
  • Wazazi wapuuziaji
  • Wazazi bubu
  • Wazazi wasinziaji
  • Wazazi wenye hatia

Wapendwa wasikilizaji, shabaha yangu ni kuelezea hizi aina za wazazi na sifa zao ili kusudi kila mzazi aweze kujifahamu kuwa je, yeye yupo katika aina ipi. Kama akijitambua kuwa yupo kwenye aina isiyotakiwa katika jamii kwenye kutoa malezi basi na ajinasue huko ili kuwa katika sehemu sahihi. Leo nitaanza kuelezea juu ya aina ya wazazi wawajibikaji kwa kujikita katika kuelezea sifa zao.

Wapendwa wasikilizaji, Wazazi wawajibikaji ni wazazi ambao wanatambua vema wajibu wao na hivyo wako tayari daima kuutimiza wajibu huo wakijua fika kuwa ni katika kutoa malezi bora, wanalijenga Kanisa la nyumbani na taifa la kesho. Wazazi wawajibikaji ni waalimu wa shule hii ya mwanzo kabisa (yaani shule ya malezi). Kipindi kilichopita nimeeleza kuwa familia ni shule ya kwanza kabisa katika kumuunda mtoto kimwili na kiroho. Katika shule hii ya awali kabisa kwa mtoto, nilieleza kuwa, waalimu wa shule hii yaani familia, ni baba mama. Kumbe, kama baba na mama ni waalimu kwenye familia zao, basi kwa hakika hawa ndio wanapaswa  kuangalia nidhamu za watoto wao, afya za watoto wao, makuzi ya watoto wao, taaluma za watoto, Imani thabiti ya kimungu wanayopaswa kuwa nayo watoto wao, kwa kutaja machache.

Ndugu zangu, baba na mama wana wajibu mwingi sana katika familia. Suala la kumlisha na kumvisha mtoto tu halimfanyi mzazi kuitwa kuwa ni muwajibikaji. Uwajibikaji upo kwenye mambo kadhaa katika familia. Pengine ningesema kuwa, familia ni kanisa la nyumbani, na viongozi wa kanisa hili la nyumbani ni baba na mama ambao ndio kwa hakika wanapaswa kuhakikisha uimara na uthabiti wa kanisa hili la nyumbani. Kama Kristo anavyotafsiriwa katika maandiko matakatifu kuwa ni kichwa cha kanisa (Rej. wakolosai 1:18), basi itoshe kusema kuwa wazazi nao wakiwa ndani ya familia ni vichwa katika kuwaongoza watoto wao kumfahamu na kumuishi Kristo.

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji, ni wale wanaotambua kuwa, familia ni shule ya sala, na kwahiyo, muda wote wanahakikisha kuwa watoto wanasali asubuhi, mchana na jioni. Ni wazazi wanaotenga muda wa kusali na watoto wao, ni wazazi wanaofundisha watoto wao kusali, ni wazazi wanaowafundisha watoto wao namna ya kukaa kwa utulivu wakati wa kusali, tena ni wazazi wanaowafundisha watoto wao kusali sala zinazotoka moyoni na si kusali kwa kutimiza wajibu wa kusali, kwani wanaelewa kuwa sala ni maongezi kati ya mtu na muumba wake. Tena, wazazi wawajibikaji ni wazazi wanaohakikisha kuwa wanasali pamoja kama familia wakiamini kuwa wanaposali pamoja Mungu anajiunga nao na kukaa mahali pale kwa wakati ule kama alivyosema; walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao. (Matayo 18:20)

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji ni wazazi wanaotambua kuwa, familia ni shule ya upendo, na kama familia ni shule ya upendo, wanajitahidi kuonyeshana upendo na kuzuia tofauti zao. Wazazi hawa wawajibikaji ambao wanatambua kuwa familia ni shule ya upendo, wanajua kuwa wao ndio waalimu wa somo la upendo kwa watoto wao. Tena upendo kwa Mungu na kwa jirani. Wazazi wawajibikaji wanahakikisha kuwa Watoto wao wanapendana wao kwa wao  katika familia, watoto wanalelewa namna ya kuwapenda majirani, ndugu na watu wote kwakuwa wanaaminishwa kuwa kila mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Rej. kitabu cha Mwanzo 1:27). Wazazi wanaowajibika kuwafundisha watoto wao, watoto wao ni wale ambao wamekuwa daima wenye kujitoa katika majukumu mbalimbali bila ya hata kujibakiza, na ndio maana wamekuwa na sifa makazini mwao. wazazi wawajibikaji katika kutoa shule ya upendo kwenye familia zao, watoto wao wanakuwa wasio na choyo, wakarimu, watoto wao hawana lugha za matusi, watoto wao wanakuwa na mahusiano mazuri na jamii zinaowazunguka, wanakuwa watatuzi wa shida za watu wengine kwa shauri zao zenye tija.

Kadhalika ni watoto wasio na hila katika maisha yao. Daima wazazi wawajibikaji katika kuwafundisha watoto wao juu ya upendo, watoto wao maisha yao yanasambaza harufu ya upendo kwa vizazi vyao. Ndo maana utasikia, ukitaka mke bora, ama mfanyakazi bora ama msimamizi mzuri wa kitu ama jambo fulani, nenda wa watoto wa mzee Joseph. Hii ni kwa sababu ya uwajibikaji mahiri wa wazazi unatengeneza mafanikio ya watoto kwa sasa na baadaye.

Kipindi hewani kipindi ni kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unayenisikiliza ni Sr Anagladness Mrumah wa Shirika la Masista Wa Usambara (COLU). Leo nimependa kuzungumzia juu ya aina ya wazazi kwenye kutoa malezi ambapo aina hizo za kiutoaji malezi zina athari hasi na chanya. Nimesema kuna aina za wazazi kama vile:

  • Wazazi wawajibikaji
  • Wazazi wa ruksa
  • Wazazi wakandamizaji
  • Wazazi wazembe na watepetevu
  • Wazazi wapuuziaji
  • Wazazi bubu
  • Wazazi wasinziaji
  • Wazazi wenye hatia

Lakini katika aina hizi, leo nimeanza na ile aina ya wazazi wawajibikaji ambayo kwa uhalisia ndiyo aina bora ambayo inapaswa kuigwa na kila mzazi katika kutoa malezi.

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji ni wale wanaotoa mafunzo ya utii kwa watoto wao wakijua kuwa, familia ni shule ya utii. Wazazi wawajibikaji ni wazazi wanaoanza kuwafundisha watoto wao utii tangu wakiwa wachanga kwa kutumia ishara na baadaye wanapoendelea kukua wanatumia maneno na matendo yanaomdai mtoto kuwa mtii. Ni wazazi wanaowajibika kuwafundisha watoto wao wawatii wao wazazi kwakuwa hata Yesu anawataka watoto kuwatii wazazi wao; Enyi watoto watiini wazazi wenu (waefeso 6:1-4). Wazazi wawajibikaji wanawafundisha watoto waonyeshe utii kati yao watoto. wazazi wawajibikaji wanawafundisha watoto kutii wakubwa na wadogo. Wazazi wawajibikaji, wanafundishwa watoto wao kuwatii waalimu mashuleni na, Zaidi sana, wazazi wawajibikaji wanawafundisha watoto wao kutofautisha utii mzuri na mbaya wakiwa wanaamini kuwa kuna watu wanaoweza kutumia dhana ya utii na kuwaathiri. Mzazi muwajibikaji anafinyanga kizazi chenye utii.

Wapendwa wasikilizaji, wazazi wawajibikaji wanafundisha watoto wao somo la uaminifu.  Daima wazazi hawa huhakikisha watoto wao ni waaminifu, wasio na hila, wenye kuridhika na walichokuwa nacho, wanawafundisha watoto wao kuzuia tabia ya udokozi, wanawafundisha watoto wao kuwa waaminifu katika misimamo yao na si kusababisha shida kwa wengine kwa ajili ya kukosa uaminifu. Wazazi wawajiikaji huhakikisha kuwa wanafuatilia taratibu kila hatua ya mtoto ili kuona kama huenda mtoto ana tabia mbaya anayoificha, ili akibaini amrudishe kwenye mstari.

Wapendwa wasikilizaji, Wazazi wawajibikaji ni shule ya fadhila nyingi.  Wanatimiza vema kazi yao wakijua kuwa wanatimiza kwa matendo sehemu ya viapo vyao vya ndoa; (Rej. Mithali 19:18, Waefeso 6:4) yaani kuwalea watoto wao kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake, huku wakiwarithisha watoto wao mila za wazee zilizo njema.

Wapendwa wasikilizaji, Wazazi wawajibikaji daima huwa na muda kwa ajili ya watoto wao. Hufuatilia kwa karibu kama watoto wametimiza wajibu zao katika elimu, au kama wamefanya vizuri katika kazi za nyumbani. Mzazi mwajibikaji humuunda mtu mzimamzima. Haishii tu kuzaa, bali huendelea kumzaa mtoto wake, kimaadili, kiimani, kielimu, kimahusiano na ki-uwajibikaji pia. Wazazi wawajibikaji, huunda watoto wenye kutimiza wajibu pia.

Kwa kuhitimisha Wapendwa wasikilizaji, hii ndiyo aina ya wazazi wawajibikaji katika kutoa malezi kwa watoto wao. Kwa hakika, nilizozitaja ndizo baadhi tu ya sifa wanazokuwa nazo wazazi wawajibikaji. Ningetamani na wewe msikilizaji wangu kutafakari kwa kina juu ya sifa hizi ili uweze kuwa mwalimu na balozi mzuri wa kusambaza sifa hizi katika jamii inayokuzunguka, kwa njia ya ushauri kwa wazazi wenzako, ili hatimaye watoto ambao ndio kizazi cha sasa na baadaye, waweze kupokea misingi imara itakayowasaidia kuwa watu wenye utu, watu timamu na watu wenye elimu ya malezi kwa watoto wao vizazi baada ya vizazi.

Tumalize kwa sala

Kwa jina la baba na la mwana na Roho Mtakatifu amina

Atukuzwe baba na mwana na Roho Mtakatifu kama mwanzo na sasa na siku zote……

Kwa jina la baba na la mwana na Roho Mtakatifu amina

 

 

Read more

MISA MAALUMU YA KUMUAGA NA KUMKARIBISHA MKURUGENZI MPYA, PIA KWA KUMALIZA KONGAMANO LA KANDA

Mnamo tarehe 20 Julai, 2025, watoto wa Utoto Mtakatifu pamoja na walezi wao kutoka parokia mbalimbali za jimbo, waliadhimisha misa takatifu kwa ajili ya shukrani kwa Mungu kwa ajili ya Kongamano la kanda ya Mashariki lililofanyika katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam tarehe 19 – 23 Juni, 2025. Maadhimisho haya yalifanyika katika parokia ya Maria Consolatha – Sua.

Sambamba na tukio hili la shukrani kwa ajili ya kongamano lililoisha, siku hii pia ilikuwa ni siku rasmi kwa ajili ya kumpongeza na kumkaribisha Padre Joachim Masangu kama mkurugenzi mpya katika Ofisi ya Mashirika ya Kipapa hapa jimboni Morogoro

Aidha, shukrani hizi ziliambatana na tukio la kumuaga Pd. Aidan Kadudu ambaye alikuwa ni mkurugenzi wa mashirika sha Kipapa Jimboni humu. Watoto katika hafla hii waliweza kucheza michezo mbalimbali kwa ajili ya kumuaga pamoja na kumpatia zawadi malimbali.

Padre Kadudu kwa sasa amehamishwa kutoka jimbo la Morogoro kuelekea jimbo la Bagamoyo. PMS Morogoro wanayofuraha kwamba padre Kadudu anaendeleza huko Bagamoyo utume wake ambao alikuwa anaufanya akiwa jimbo la Morogoro wa kusimamia na kuliendeleza shirika la utoto mtakatifu jimboni humo.

 

 

 

 

Imeandaliwa na: Pd. Joachim Masangu, Mkurugenzi PMS Jimbo

 

 

Read more

WAZAZI WASAIDIENI WATOTO KUZIISHI AMRI ZA MUNGU NA ZA KANISA

Sala: Kwa Jina la Baba na la Mwana nala Roho Mtakatifu Amina.

Salamu Maria umejaa neema, bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa/ Maria mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu Amina.

Bikira Maria Malkia wa Familia, Utuombee

Kwa jina la baba na la mwana na la Roho mtakatifu amina.

Kutoka hapa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unayenisikiliza muda huu ni mimi Sr Anagladness Mrumah, ambaye ni Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa.

Wapendwa wasikilizaji wa Redio Maria Sauti ya kikristo nyumbani mwako pamoja na mshirika wake Redio Mbiu kutoka Bunena, leo napenda Kuwaasa Wazazi kuwasaidia Watoto wao kuziishi Amri za Mungu na za Kanisa kwani inaonekana hii ni changamoto kwa wazazi wengi. watoto wanaishia kuzifundishwa hizi amri kwenye mafundisho yao huko kanisani tu, wakifika nyumbani wazazi hawana habari kwamba ndio wanaopaswa kuhakikisha kuwa watoto wanaziishi hizi amri.

 

Wapendwa wasikilizaji, pengine imekuwa sasa ni tabia ya sisi wazazi kuona kuwa ni wajibu wa viongozi wa kanisa kufundisha juu ya amri za mungu na za kanisa kwa watoto wetu, ingawaje hata sisi wazazi tayari tunazifahamu. Haidhuru hata kama ni wajibu wao viongozi wa kanisa kuzielezea kwa watoto wetu, lakini watoto wamekuwa wengi wao wanakengeuka yaani hawazishiki wala kuziishi vyema kwani sisi wazazi tumeshindwa kuwasisitiza ili waweze kuziishi ndani ya familia zetu.

 

Wapendwa wasikilizaji, wengi wetu tunashindwa kuwakazania watoto wetu waziishi vyema amri za Mungu na za Kanisa, kwakuwa sisi nasi tumeshindwa kuziishi. Hii ndiyo sababu tunashindwa kusisitiza, kitu ambacho wenyewe hatukiishi. Kwamfano, amri ya kwanza ya kanisa inayosema, Hudhuria Misa Takatifu na Dominika zilizoamriwa! Sasa kama mzazi mwenyewe mlango wa kanisa anauona kama kituo cha polisi, je, ataweza kumsisitiza mwanae juu ya amri hii ya kuhudhuria misa takatifu? Je kama katika umri huo alionao mzazi hajaona thamani ya maadhimisho ya misa takatifu ambayo ni kilele ya ibada zote, ataonaje ulazima wa kumlea mtoto katika kutambua kwa matendo thamani ya kuhudhuria misa takatifu? Jibu ni haiwezekani kwakuwa mtu hutoa kile alichonacho moyoni mwake. Ndugu zangu kuhusu kuhudhuria misa ama kutokuhudhuria misa kwa mtoto, hilo ni jukumu la mzazi. Kwahiyo tuwahimize waende kanisani, tusisubiri mapadre wakahimize watoto kufika kanisani wakati sisi ndio viongozi wa familia ambao tuna wajibu wote wa kutekeleza jukumu hili. Na ndugu zangu wazazi, niseme tu kwamba, kama sisi tunaonekana kupuuzia mambo haya matakatifu, ndio maana hata watoto mara nyigine wanalegea katika Imani kwani daima mtoto anaangalia na kuiga kile kinachofanywa na mzazi.

 

Vile vile wapendwa wasikilizaji, ni vyema sisi kuwasisitizia watoto wetu hasa wale ambao wameshapata komunyo ya kwanza, kupokea ekaristi ambayo ni amri ya kanisa, tena wakiwa wamejiandaa vyema kwani ekaristi takatifu ni Yesu Kristo mwenyewe. (Rejea Mt 26:26-28) Ni chakula cha kipekee kuliko vyakula vyote tunavyokula katika maisha yetu. Ekaristi takatifu ni uzima wetu, ni dawa ya kiroho. Ingekuwa vizuri kama mzazi angeona njaa ya kiroho kama hakupata nafasi ya kupokea ekaristi takatifu. lingekuwa ni jambo la maana kama mzazi naye angeendelea kumkazia mtoto juu ya thamani ya Ekaristi Takatifu. lingekuwa ni jambo la busara kama mzazi kabla mtoto hajaenda kanisani, angepata wakati wa kumkumbushia namna ya kupokea ekaristi takatifu viganjani. Tena Lingekuwa jambo jema kama mzazi angeweza mara kwa mara kumkumbushia mwanae kumwambia yesu maombi yake wakati anapokula mwili wa Kristo yaani ekaristi katatifu. Sishangai kwamba wengi wetu tunashindwa kuyafanya haya yote kwakuwa sisi nasi hatuioni thamani ya ekaristi takatifu na pengine hatushiriki hii ekaristi.

 

Kwanini, kwasababu eti mzazi ametenda dhambi na hataki kuiungama wazi na hii kumpelekea kukosa huduma hii muhimu ya kiroho. Wengine tumekuwa tukikubali kuchanganywa na madhehebu ambayo yanapinga uwepo wa Yesu ndani ya Hostia Takatifu. Sasa kwakuwa mzazi anakubali kuchanganywa, basi naye anakosa ujasiri wa kuhamasisha wanae juu ya ukuu wa ekaristi takatifu, na hivyo kufanya watoto kukosa mwamko katika kuyashiriki matakatifu. Na pengine mzazi mwingine ni mvivu wa kwenda kanisani na kwahiyo hapati hii nafasi ya kushiriki ekaristi takatifu. Na wengine wanajishikilia sana na shughuli za ulimwengu huu pasipokuona kuwa ipo haja ya kutenga siku moja hii muhimu kwa ajili ya Mungu na hivyo kuweza kuiishi amri ya tatu ya Mungu inayosema, Shika Kitakatifu Siku ya Mungu. (Kumb 5:12)

 

Mbaya zaidi wapendwa wasikilizaji, wengine kwakuwa siku za katikati ya wiki alikuwa amebanwa na shughuli, basi anaona kuwa jumapili niya mapumziko. Ndio ni ya mapumziko ila kwa mkristo mkatoliki mapumziko kwa siku ya jumpili yanaanza mara baada ya kushiriki misa takatifu. Kumbe ndugu zangu wazazi, baada ya mtoto wako kupokea mafundisho juu ya namna ya kupokea ekaristi, shule ya nyumbani ndiyo inapaswa kuchukua mkondo wake wa kuendelea kuhamasisha matakatifu kwa watoto wetu. Vitu hivi tungevifanya sisi wazazi kama majukumu ya mzazi kwa mtoto wake, hakika kiroho watoto wetu wangekuwa mbali. Sasa sisi tumezoea kwamba mtoto akishamaliza mafundisho ya sakramenti husika inatosha, Jambo ambalo si sahihi. Kwa hulka ya mwanadamu ili akili yake iweze kukaa sawa, ni lazima akumbushwe mara nyingi juu ya jambo muhimu, ili jambo lile liweze kumkaa kama sehemu ya maisha yake.

 

Wapendwa wasikilizaji, hebu ona umuhimu wa wewe kumfundisha mtoto wako juu ya kutoa zaka. Pengine utasema kwamba zaka ni fungu la kumi la pato la mtu na mtoto hana pato kwakuwa anakutegemea wewe mzazi. Lakini ndugu zangu wazazi, hebu jaribu kumshirikisha mtoto kwamba kama unampatia shilingi elfu moja, basi mia moja amtolee mungu kama zaka yake. Lengo msingi hapa ni kumzoeza mtoto kufahamu au kupata uelewa huu akingali mdogo ili akishakuwa mkubwa na kumiliki hela yake mwenyewe, awe tayari anajua kuwa kama mwanakanisa anapaswa kutoa zaka kwani hii ni amri ya tano ya kanisa. Tusiwaache hawa watoto wakaziimba tu hizi amri pasipo kuzielewa kwa undani.

 

Kwamfano mtoto kila asubuhi na jioni anaimba amri ya tatu ya Mungu, Ungama dhambi zako walau mara moja kwa mwaka. Lakini tangu mtoto wako alipoungama akiwa anapata komunio ya kwanza, hakuwahi tena kuliona sanduku la maungamo. Kwanini, kwasababu wewe mzazi unaona hilo sio jukumu lako la kujua kwamba mtoto anaendeleaje kiroho. Kumbe katika udogo wake, hata akimpiga mwenzake, akiiba sukari, akitukana watu, ungeweza kumsihi aende kuungama! Hii ingemfanya aiishi amri ya 3 ya kanisa! Familia ni shule jamani, na waalimu ni wewe baba na mama

 

Wapendwa wasikilizaji, kama sisi wazazi tungekuwa tunawasisitiza sana watoto wetu kujihami juu ya uvunjifu wa amri za Mungu kwa mfano amri ya  ya tano ya mungu inayosema USIUE, hakika tusingeshuhudia mauaji ya kiroho ama ya kimwili ambayo yamekuwa yakitendeka hapa na pale, kwani mtu anayethubutu kuua mwingine kiroho kwa maneno yake machafu ambayo yanaweza kumchafua mwingine nahata kushusha hadhi yake, au kimwili yaani kuutoa uhai wake, huyu ni yule ambaye hajui athari ya kuua wala thamani ya utu wa mtu mwingine. Na mtu yeyote anayefanya kitendo hicho ni yule ambaye hakufundwa na wazazi wake na ndio maana anaweza kuona tu kwamba ni jambo la kawaida. Ndio maana wazazi, leo nimeamua nizungumzie juu ya jambo hili kwani tumekuwa tukikariri amri za mungu na za kanisa lakini wengi wetu hatuziweki katika matendo. Ni jukumu letu wazazi kuwasisitiza watoto wetu juu ya kuyaacha yale matendo ambayo mungu ameyakataa kwani hayo ni chukizo kwake. Kama watoto watakuwa wanakuwa na hofu ya Mungu na kuona kuwa jambo baya hawapaswi kulitenda pindi wakiwa wadogo, basi vitendo viovu havitaweze kutendeka katika jamii zetu. Lakini kama tutasubiri makatekista, masista na mapadre wafundishe na halafu itoshe, basi tutakuwa tunapoteza vizazi vya mbele yetu, kwani wahimizaji wa mambo haya ni sisi wazazi ambao tunaweza kufuatilia mienendo yao siku zote kwani wao ni sehemu ya familia zetu.

 

Kipindi hewani ni kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unayenisikiliza muda huu ni mimi, Sr Anagladness Mrumah. Ndugu zangu wasikilizaji leo nimeamua kuwasisitiza wazazi kuhakikisha kuwa wanawahimiza watoto kuzishika na kuziishi amri za Mungu na za kanisa barabara kwakuwa amri hizi baada ya kufundishwa kwenye mafundisho, hazishikwi barabara kwa kuwa wazazi walio wengi hawawahamashishi watoto kuziishi wala kuziishi.

 

Ndugu zangu wazazi, kama sisi wazazi tungewasisitiza watoto wetu juu ya kushikilia amri za mungu tungeweza kuzuia maovu mengi. Kwamfano, kama unaona mtoto ana hali ya udokozi, ingekuwa ni vizuri kumkumbusha kwa kumsisitiza kuwa asirudie tena kwani ni amri ya saba ya mungu. Kwa msisitizo kama anajua kusoma unafungua biblia kabisa aone kwamba ni kweli kumbukumbu la torati sura ya 5:19 Mungu anasema usiibe. Yaani asione tu kwamba ni amri yako wewe unayompa ya kutofanya kitendo kile, bali kwamba ni amri kutoka kwa mungu kwamba kuiba hakuruhusiwi kabisa. Sasa sisi tunalea pasipo kuonyesha rejea kwenye mambo matakatifu ambapo mtoto angeweza kushikilia vizuri zaidi baada ya kujua kuwa mzazi na mungu hawataki jambo la kuiba kwani ni baya. Ndugu zangu hakuna mtu anayeweza kuiba kama katika maisha ya utoto wake aliaswa kwamba jambo hili ni chukizo kwa Mungu. Kwahivyo tuwahimize watoto kuziishi amri za mungu, wasikariri tu.

 

Wapendwa wasikilizaji matendo ya uovu kama yale ya kusema uongo, usaliti kwenye ndoa ama uvunjifu wa ndoa visingekuwapo kama sisi wazazi tungekuwa tuko mstari wa mbele kuwalea watoto wetu katika kushikilia mambo kama hayo. Tazama leo watu wanazushiana uongo hata wa kuingizana jela, au kuua dhamiri za wengine kwa maneno yao ya uongo. Kwanini? Kwakuwa hawana hofu ya Mungu. Wazazi wao hawawazi wala kukaa na kuwahimiza watoto wao kuwa wasijethubutu kuyatenda hata kabla hayajatukia. Wazazi wengine kwa uongo wameshawarithisha watoto wao hadi mtoto anaona uongo ni sehemu ya maslahi au mafanikio yake. Mtoto mwingine anashindwa kutulia kwenye ndoa yake, awe wa kiume ama wa kike kwakuwa mzazi hakuwahi kukemea kabla. Na pengine wazazi nao wanashindwa kuzungumzia hayo kwakuwa baba na mama wote ni wasaliti wa amri hiyo ya mungu. Kwahiyo kwa mantiki hii watoto wanashindwa kushika amri ya nane ya mungu inayosema Usiseme Uongo kwani wazazi hawako tayari kulizungumzia jambo hilo kwakuwa nao wapo kwenye shimo hilo hilo la uongo, wala kukemea juu ya usaliti kwani wamekuwa wakiuendesha usaliti ama bado wameukumbatia.

 

Kwahiyo ndugu zangu wasikilizaji wa Redio Maria na mshirika wake Redio Mbiu, tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa na watoto wetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa amri za mungu na za kanisa zinashikwa. Tukumbuke kuwa mtoto anaposikia na kutenda, jambo hilo linakaa akilini zaidi na hivyo kulichukua kama sehemu ya maisha yake ya kila siku. Kwamfano, kama mtoto amesikia juu ya amri sita za kanisa na halafu mzazi akawa wa kwanza kumsaidia kuziishi kwa kumshirikisha kiutekelezaji, hakika mtoto hata akiwa mtu mzima hataacha kushika amri za kanisa. Ee, ataenda kanisani, atapokea ekaristi kama ameshapokea sakramenti ya ekaristi, atatoa zaka kama mzazi amekuwa akimtolea na kumwelewesha maana yake, na amri zote za kanisa

 

Hali kadhalika, kama mzazi atamsisitiza mtoto wake kushika amri za Mungu, mtoto ataweza kutambua kuwa ni yapi Mungu anamtaka ayafuate na ni yapi anamkataza asiyafanye. Hebu wazazi tusome tena amri za Mungu ambazo zinapatikana katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:1-21 ili tuone maagizo haya kutoka kwa Mungu. Kwa kweli mimi naamini kwamba kama mtoto hazishiki amri za Mungu kwasababu ya uzembe wa mzazi, basi mzazi huyo ndiye anayeathirika kwanza kabla ya jamii. Maana, Amri hizi tumepewa na Mungu tuzishike illi zitusaidie kuishi kwanza kitakatifu na pili kiadilifu katika familia na jamii zetu. Kama hatuzizingatii tutakuwa tunafuga katika jamii watu wezi, waongo, wasio na heshima, wasaliti, washirikina, wauaji na wasiojua wajibu wao ndani ya kanisa lao. Kwa leo ni haya nilipenda wasikilizaji wa Redio Maria na Mshirika wake Redio Mbiu tujikumbushie.

 

Ni mimi mtangazaji wako Sr Anagladness Mrumah kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)

 

 

Read more

SAFARI KUELEKEA DAR ES SALAAM KWENYE KONGAMANO LA UTOTO MTAKATIFU KANDA YA MASHARIKI (DSM)

Mnamo tarehe 19 Juni 2025, zaidi ya watoto 100 kutoka jimbo la Morogoro walifanikiwa kuanza safari yao ya kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya Kushiriki Kongamano la kanda ya mashariki la utoto Mtakatifu ambalo lilikuwa na jumla ya watoto 2567. Aidha, kongamano hili lilijumuishwa na majimbo saba ambayo ni: Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Bagamoyo, Zanzibar, Morogoro, Ifakara, Mahenge, na Tanga.

Kongamano hili lilifanyika katika parokia ya Kristo Mfalme Tabata DSM. Watoto walisafiri kwa njia ya Gari Moshi (Treni). Safari hii kwa watoto ilikuwa ya furaha sana kwani takribani watoto washiriki wote, hii ilikuwa mara yao ya kwanza kusafiri na chombo hiki cha kisasa hapa nchini. Kongamano lilikuwa zuri kwa watoto kwani waliweza kujifunza mambo mengi kwa kipindi chote cha siku tano yaani tarehe 109 23 Juni 2025.

Aliyeadhimisha misa ya ufunguzi alikuwa ni Askofu msaidizi wa jimbo kuu la Dar es Salaam, Henry Mchamungu, akiongozana na mapadre wakurugeni kutoka kanda ya DSM; Pd. Joachim Masangu (Morogoro), Pd. Denis Wigira (Dar es Salaam), Pd. Aidan Kadudu (Bagamoyo), Pd. Haki (Zanzibar), Pd. Julius Mgaichuma (Mahenge), Pd. Michael Mhina (Ifakara), Pd. Paul Semng’indo (Tanga)

Sukrani kwa Mungu kwa kutusafirisha salama. mwenyezi Mungu na awasaidie watoto wetu waendelee kukua katika kumjua Mungu na pia kuwa na ari zaidi ya kuyatimiza matakwa yake.

 

 

 

Imetayarishwa na Pd. Joachim Masangu, Mkurugenzi PMS

 

Read more

TAARIFA YA KONGAMANO LA UTOTO MTAKATIFU JIMBO LA NJOMBE, 24-28 JUNI, 2025

Kongamano lilikuwa kwa ajili ya kuadhimisha jubilei ya watoto katika mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu 2025. Watoto washiriki walikuwa 2500. Walezi 11, masista 12, mapadre 9, mashemasi 3 na waseminari wawili wa mwaka wa uchungaji Mada zilizofundishwa: 1. Jubilei Kuu 2025, 2. Liturjia Katoliki,3. Lishe. 4. Ulinzi na usalama wa mtoto Majina ya watoa mada: Fr. Erasmo Mligo, Fr, Gabriel Haule, Bi. Bertha Bartholomeo Nyigu, Bi. Alodia Mkinga

Aidha, Kwenda kwenye eneo  la  kongamano  kila  parokia  walitakiwa  kuwafikisha watoto Sekondari ya Josefine. Kwa kulingana na Jografia ya jimbo letu, Parokia za mwambao wa ziwa walianza safari kwa  boti mpaka  kufika  nchi kavu na hatimaye kwa mabasi mpaka eneo la kongamano. Parokia nyingine walikodi mabasi yaliyowaleta mpaka eneo la kongamano. Siku ya kilele, ilitia fora sana. Watoto, masista wachache na walezi waliandamana wakisindikizwa na polisi wa usalama barabarani mpaka jimboni. Baada ya misa walirejea eneo la kongamano  kwa  sherehe za kufunga na hatimaye kurudi Parokiani.

Ni ukweli usiopingika kuwa Watoto walifurahi sana kukutana kama watoto wa jimbo moja na kufanya mambo mbalimbali pamoja. Misa ya ufunguzi wa kongamano iliongozwa na Mkurugenzi wa utume wa Walei Jimbo la Njombe Mhesh Padre Francisco Betes Chengula. Misa ya kufunga kongamano iliongozwa na Mhashamu Eusebio Samwel Kyando. 10. Watoto waliagizwa kusoma lnjili yote ya Yohane na kutoka humo walikuwa na mashindano ya kujibu maswali. Aidha, kulikuwa na mashindano ya lgizo lililotoka katika lnjili hiyohiyo na shindano la Kwaya.Wimbo ulioshindaniwa umefanywa kuwa Wimbo wa Utoto Mtakatifu Jimbo Katoliki la Njombe kwani watoto wote jimbo zima wanaweza kuuimba. Baada ya mashindano tuliutangaza rasmi kuwa ndio wimbo wa Utoto Mt Jimbo. Tuliagiza kila Parokia watoto wakutananpo kwa sala au michezo uimbwe kwanza. Kulikuwa pia na ngoma za asili za burudani toka Ukisi,Mwambao wa Ziwa Nyasa, Upangwa na Ubena.

Kongamano letu halikuwa la kikanda . llikuwa ni jubi lei ya watoto wa jimbo la Njombe katika mwaka Mtakatifu ambapo makundi mbalimbali ya kikanisa wanaaadhimisha mfano mapadre, watawa, wana ndoa, vijana ,wasemi nari nk. Sasa kwa upande wa watoto imefanyika ushiriki na ufanisi mkubwa zaidi- ya kundi lolote. Parokia zote SO za jimbo zilikuwa na wawakilishi. Ohamira ya kongamano ikiwa ‘mletee mtoto katika njia ipasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee’ Mith 22:6. Mimi kama mlezi nilifurahiswa zaidi na mambo matatu; kwanza ushiriki mkubwa wa watoto. Pili, watoto walivyofurahi hasa siku ya kilele licha ya baridi kali ya Njombe na tatu, jinsi watoto walivyochangamkia mada walizokuwa wanafundishwa hasa mada iliyohusu ulinzi na usalama wao.

Tunamshukuru sana Mungu kwa kutuwezesha kufanya kazi hii iliyotukuka ya kimisionari; bila kupata changamoto ya pekee. Pili, tunamshukuru sana Mhashamu Baba Askofu Kyando kwa kuruhusu niitishe kongamano hili iii kuweka alama katika mwaka huu wa Jubilei Kuu 2025 . Nawashukuru mapadlre, watawa, makatekista,walezi wa watoto na waza zi kwa maandaliz i yote waliyofanya hata kunifanya nionekane nimefaulu; kwa kweli wao ndio waliofaulu. Mimi nilikuwa mratibu tu. Mwisho, lakini si kwa umuhimu nawashukuru Ofisi ya PMS Taifa kwa kutuhamasisha kufanya shughuli hizi iii kung’arisha umisionari wa watoto. Hamasa yenu ndiyo iliyonisukuwa kujasiria mambo haya matakatifu.

 

 

 

Imetayarishwa na: Pd. Julius Mgaya, Mkurugenzi PMS Jimbo

 

 

 

 

 

 

Read more