Katika Jimbo Kuu Katoliki Songea, shirika la Utoto Mtakatifu lipo hai na linaendelea vizuri katika kutekeleza utume wake, kwani idadi ya watoto wanaojiunga na shirika inaongezeka kila mwaka. Ongezeko hili la watoto limetokana na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na walezi kuanzia ngazi ya jumuiya mpaka Jimbo. Elimu imetolewa kwa Mapadre, Watawa, wazazi na kwa kanisa nzima juu ya malezi kwa watoto wetu ambo ni kanisa la kesho. Kila mmoja anao wajibu wa kuwalea watoto wetu kimwili na kiroho ili waweze kusimama imara katika kanisa kwa kuilinda imani yao.
Watoto wanafundishwa kuwa watu wa sala daima ambayo kimsingi ndiyo hatua ya kwanza ya kuwa wamisionari. Wanafundishwa kuwa na imani thabiti ili kuwajengea roho ya kimisionari kwa watoto wenzao. Wanafundishwa pia namna ya kujitoa kwa Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana na Mwokozi wao. Wanafundishwa kuwa wakarimu kwa watu wengine huku wakiongozwa na kauli mbiu yao “watoto kuwasaidia watoto wenzao”. Hata hivyo bado kuna mtazamo hasi kwa baadhi ya wazazi ambao hudhani ya kuwa Utoto Mtakatifu ni kwa ajili ya watoto wa kike tu, mtazamo ambao umesababisha kuwa na idadi ndogo ya watoto wa kiume katika shirika. Jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuondoa mawazo haya potofu ya baadhi ya wazazi na walezi ikiwa ni pamoja na kutoa semina ya malezi bora kwa wazazi.
MAADHIMISHO YA SIKU YA UTOTO MTAKATIFU
Sherehe za watoto mashahidi yaani tarehe 28 Desemba hufanyika kila mwaka katika Jimbo letu. Hata hivyo sherehe hizi za Utoto Mtakatifu hazikufanyika katika ngazi ya Jimbo bali kila parokia husherehekea kadiri ya nafasi. Parokia zilizo nyingi huadhimisha sherehe za utoto Mtakatifu kuanzia tarehe 28/12 hadi tarehe 31 Desemba na siyo baada ya tarehe hizo tajwa hapo juu. Katika sherehe hizi watoto hufundishwa mada mbalimbali za kujitoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu wakiwaiga watoto mashahidi.
KAZI WANAZO FANYA WATOTO
Watoto jimboni hujishughulisha na kazi mbalimbali kwa ajili ya malezi yao wenyewe kama vile; makongamano ngazi ya Parokia, Dekania na Jimbo, Misa Takatifu, michezo mbalimbali , usafi , kuimba nyimbo zenye ujumbe maalumu kwa watoto wenzao na kwa jamii inayo wazunguka.
MBINU ZINAZOTUMIKA KUWAFUNDISHA WATOTO
Kuna mbinu nyingi zinazotumika katika kutoa elimu kwa watoto wetu nazo ni kama zifuatazo; Biblia takatifu, vitabu vyenye historia za watakatifu, masimulizi mbalimbali, michoro na picha.
UONGOZI WA WATOTO
Kuhusu viongozi wa watoto Jimboni, watoto wetu ndani ya Jimbo kuu katoliki Songea wanao uongozi wa parokia na Jimbo yaani, mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, katibu msaidizi na mtunza hazina. Umri wa watoto walioko ndani ya shirika ni kuanzia miaka saba hadi kumi na minne.
KALENDA YA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA
Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa mwongozo wa kalenda iliyosheheni shughuli za watoto tunayopewa kutoka ofisi ya mashirika ya kipapa taifa. Mwongozo huu wa kalenda ni msaada mkubwa kwa walezi katika utume wao wa kuwalea watoto. Kalenda hii inasaidia kujua nini kinatakiwa kufanyika kila siku kwa watoto. Kila mmoja wetu analo jukumu la kuhakikisha kila mtoto anapewa ulinzi na usalama kwani hizi ndizo haki msingi za watoto. Ujumbe tuwalinde watoto wetu kwani hawana mtetezi, jukumu la ulinzi kwa watoto ni la kila mtu mzima .
KITABU CHA MBINU ZA KUWALEA WATOTO
Kitabu hiki cha mwongozo wa namna ya kuwalea watoto na walezi kinatumika vizuri sana tena ni msaada mkubwa kwa malezi. Hata hivyo tungependa kushauri kuwa iongezwe mada moja kwa ajili ya wazazi peke yao ili iwasaidie kujitambua. Wapo baadhi ya wazazi ambao hawajui kabisa umuhimu wa kuwaruhusu watoto wao ili wajiunge na watoto wenzao. Endapo wazazi wataelimishwa itakuwa ni njia nzuri ya kuwapata watoto wengi wanaojiunga na shirika.
MICHANGO YA UTOTO MTAKATIFU
Ili kuongeza ukarimu wa michango ya utoto mtakatifu ofisi yetu imefanya jitihada mbalimbali kama vile kutuma timu ya wahamasishaji kwenye parokia zetu za jimbo, kugawa bahasha maalumu kwa watu binafsi, familia na kwenye jumuiya zetu ndogondogo za kikristo ambapo waamini huweka ukarimu wao na kujipatia baraka. Kila parokia huombwa kiwango cha ukarimu kadiri ya moyo wa watu kwani kutoa siyo utajiri bali ni moyo wa mtu binafsi unaosukumwa na upendo wa Mungu.
Imetayarishwa na: Pd. Siliverius Nziku, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo